Wanasoka wa Bayern Munich watamalaki tuzo za Uefa
Na MASHIRIKA
FOWADI matata wa Bayern Munich, Robert Lewandowski, 32, ametawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka 2019-20 katika tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) mnamo Oktoba 1, 2020.
Lewandowski ambaye ni nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Poland, aliwapiku kipa Manuel Neuer wa Bayern na kiungo wa Manchester City, Kevin de Bruyne.
Mkufunzi Hansi Flick wa Bayern alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka baada ya kumpiga kumbo Julian Nagelsmann wa RB Leipzig na Jurgen Klopp aliyeongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya miaka 30.
Kutawazwa kwa Flick kulichangiwa na mafanikio yake ya kuongoza Bayern kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita. Ilikuw amara ya sita kwa Bayern kutia kapuni taji hilo.
Lewandowski alifunga jumla ya mabao 55 kutokana na mechi 47 za msimu uliopita huku Bayern wakinyanyua mataji matatu kwa mkupuo – UEFA, Bundesliga na German Cup.
Fowadi huyo alifunga mabao 16 zaidi kuliko mwanasoka mwingine yeyote miongoni mwa vikosi vyote vya ligi tano kuu za bara Ulaya; yaani Serie A (Italia), Ligue 1 (Ufaransa), EPL (Uingereza), La Liga (Uhispania) na Bundesliga (Ujerumani) katika mashindano yote ya 2019-20.
Fowadi Pernille Harder wa Chelsea alitawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.
De Bruyne, 29, alitawazwa Kiungo Bora wa Mwaka katika UEFA na kuvunja ukiritimba wa Bayern kwenye tuzo hizo kwa upande wa wanaume mwaka huu.
De Bruyne ambaye ni raia wa Ubelgiji, alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika tuzo za Chama cha Wanasoka wa Kitaaluma (PFA) mwanzoni mwa Septemba 2020.
Neuer, 34, ambaye pia ni mlinda-lango wa timu ya taifa ya Ujerumani, alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka baada ya kutofungwa bao katika jumla ya mechi sita za UEFA. Umahiri wa Neuer langoni pa Bayern ulisaidia waajiri wake kupiga Paris St-Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo Agosti 23, 2020 jijini Lisbon Ureno.
Joshua Kimmich, 25, wa Bayern alituzwa Beki Bora wa Mwaka wa 2019-20.
Flick, 55, aliyekuwa kocha msaidizi wa Bayern, alipokezwa mikoba ya kunoa miamba hao wa soka ya Ujerumani na bara Ulaya mnamo Novemba 2019 baada ya kutimuliwa kwa mkufunzi Niko Kovac kwa sababu ya matokeo duni yaliyosajiliwa na waajiri wake mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.
Nyota wa zamani wa Chelsea na Ivory Coast, fowadi Didier Drogba alitwaa tuzo ya Rais wa Uefa, Aleksander Ceferin kwa juhudi zake za kuchangia maendeleo ya soka na kujitolea kwake kukuza wanasoka chipukizi ndani na nje ya uwanja.
Tuzo za Uefa kwa wakati mmoja na droo ya mechi za makundi katika kipute cha UEFA msimu huu jijini Geneva, Uswisi. Kura kwa minajili ya kuchagua Wanasoka Bora wa Mwaka zilipigwa na jumla ya wakufunzi 80 walioongoza vikosi vyao kushiriki kampeni za UEFA na Europa League msimu uliopita wa 2019-20 kwa pamoja na wanahabari 55 kutoka kwa mataifa wanachama wa Uefa.
TUZO ZA UEFA ZA MWANASOKA BORA WA MWAKA 2019-20:
Mchezaji Bora wa Mwaka – Robert Lewandowski (Bayern Munich)
Kocha Bora wa Mwaka – Hansi Flick (Bayern Munich)
Kipa Bora wa Mwaka – Manuel Neuer (Bayern Munich)
Beki Bora wa Mwaka – Joshua Kimmich (Bayern Munich)
Kiungo Bora wa Mwaka – Kevin de Bruyne (Manchester City)
Fowadi Bora wa Mwaka – Robert Lewandowski (Bayern Munich)
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO