Wanasoka wa mashinani wapata fursa ya kuchuana na wabunge
NA RICHARD MAOSI
Ziara ya siku tatu ya wabunge katika kaunti ya Nakuru, ukanda wa kati tawi la magharibi, ilinoga wachezaji walipopata nafasi ya kuchuana na wabunge..
Waandalizi wa michuano hii wakiongozwa na kiongozi wa vijana bungeni Bw Gideon Keter,waliwaleta pamoja vijana wa mitaa,wanaochezea timu mbalimbali mashinani katika hatua ya kuinua vipaji,kupiga teke utumizi wa mihadarati na ukosefu wa ajira.
Siku ya Ijumaa Bunge FC walifungua kampeni yao dhidi ya Central Rift Refrees,Jumamosi wakapiga na Central Rift Officials kabla ya kukabana koo na Nakuru Wazee siku ya Jumapili ugani Afraha.
Japo Bunge FC walikosa mshambulizi wao mahiri mheshimiwa Kipchumba Murkomen walitumia huduma za mbunge wa Nyali Mohammed Ali akishirikiana na mbunge wa Nakuru David Gikaria.
Kando na hayo wabunge walizuru eneo la Kuresoi kusini na baadaye kaunti ya Bomet kushiriki mechi na timu ya vijana ya Ararwet,Young Stars na kisha wakafunga kazi dhidi ya Chemaner FC.Keter aliwaomba vijana kujiepusha na uhalifu na kukumbatia michezo kama njia ya utangamano.
“Vijana hawajawekwa kando katika ajenda za serikali, hao ndio viongozi wa kesho.Wajitume na kuhakikisha mafanikio ya kesho yanawategemea katika asilimia kubwa,”Keter alisema akizungumza na taifa Leo.
Hili linajiri mwezi mmoja tangu timu zinazoshiriki michuano ya ligi ya FKF kuboreshewa uwanja wa Afraha na gavana Lee Kinyanjui
Mbali na kutoa mipira nyavu mabuti na jezi kwa timu kadhaa,mkufunzi wa Bunge FC George Sunguti aliwahakikishia vijana kwamba ameanzisha hatua ya kutafuta vipaji mashinani kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa ambayo imevalia njuga swala hilo.