Michezo

MALIPO DUNI: Wanasoka wanawake timu ya taifa ya Amerika wakata rufaa

May 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake nchini Amerika imekata rufaa dhidi ya maamuzi ya mahakama kuu iliyotupa kesi yao ya kudai kiwango sawa cha malipo ambayo hutolewa kwa timu ya taifa ya wanaume nchini humo.

Kesi hiyo iliyowasilishwa na wanasoka 28 wa timu ya taifa ya USA ilitupwa mapema wiki jana na jaji wa mahakama kuu nchini Amerika, Gary Klausner.

Katika kesi hiyo dhidi ya Shirikisho la Soka la Amerika (USSF), wachezaji hao walikuwa wakidai fidia ya takriban Sh7.4 bilioni ambazo kwa mujibu wao, wamekuwa wakinyimwa tangu kutekelezwa kwa kanuni mpya za malipo sawa kwa wanasoka wa USA mnamo 2018.

Molly Levinson ambaye ni msemaji wa timu ya taifa ya wanawake ya USA amethibitisha kuwasilishwa kwa rufaa yao kortini.

“Malipo sawa kwa wanasoka yamaanisha kuwapa wanasoka wa kike malipo na marupurupu sawa na yale ambayo wachezaji wa kiume hupokezwa kwa shughuli ile ile ya kusakata soka uwanjani kwa kipindi cha dakika 90,” akatanguliza Levinson.

“Madai kwamba wanasoka wa kike wa USA hulipwa vyema kwa kupokezwa marupurupu yanayokaribiana na yale ambayo wenzetu wa kiume hupata kila mara hata kama hawatii fora katika mapambano yao hayana msingi.”

“Madai hayo yanakosa mashiko zaidi wakati ambapo timu ya wanawake ndiyo inayojivunia ufanisi wa kuandikisha ushindi katika idadi kubwa zaidi ya mechi za kimataifa kuliko kikosi cha wanaume,” akaongeza kinara huyo.

Akitoa maamuzi yake wiki iliyopita, Klausner alisema: “Kikosi cha wanawake kimelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha za jumla kutokana na wingi wa mafanikio yake katika mashindano mbalimbali. Tuzo za kifedha pekee ambazo zimetolewa kwa timu ya wanawake ya USA ni zaidi ya maradufu ya malipo ambayo kikosi cha wanaume kimewahi kupata katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.”

Ingawa hivyo, jaji huyo alidumisha kesi inayolalamikia kubaguliwa kwa wanasoka wa kike katika kiwango cha marupurupu ya usafiri, makazi na bima ya afya. Anatarajiwa kuiamua kesi hiyo mnamo Juni 16, 2020, jijini Los Angeles.

Timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini USA ilijinyakulia taji la Kombe la Dunia kwa mara ya nne mfululizo mwaka jana. Isitoshe, inajivunia kunyanyua nishani ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki mara tano.

Kwa upande wao, wanasoka wa kiume wa USA waliwahi kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002. Ufanisi wao mkubwa zaidi katika ulingo wa soka ni kukamilisha fainali za Kombe la Dunia katika nafasi ya tatu mnamo 1930 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Carlos Cordeiro ambaye ni rais wa zamani wa USSF, alijiuzulu mnamo Machi 2019 baada ya kesi hiyo ya timu ya taifa ya wanawake ya USA kuwasilishwa mahakamani.