• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Wanataekwondo wa kwanza kabisa wa Kenya katika Olimpiki walienda wapi?

Wanataekwondo wa kwanza kabisa wa Kenya katika Olimpiki walienda wapi?

Na GEOFFREY ANENE

MILDRED Akinyi Alango na Dickson Wamwiri Wanjiku walikuwa Wakenya wa kwanza kabisa kupeperusha bendera ya Kenya kwenye mashindano ya Olimpiki katika mchezo wa taekwondo.

Akinyi na Wamwiri walikuwa machipukizi waliposhiriki Olimpiki za Beijing nchini Uchina mwaka 2008 katika uzani wa kilo 49 na 58 mtawalia.

Milka, ambalo ni jina Akinyi analofahamika nalo zaidi, alibanduliwa nje na Wu Jingyu kutoka China naye Wamwiri akaondolewa na Chu Mu-yen kutoka Chinese Taipei katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza.

Wakenya hao wanaaminika kuvuna tuzo ya kati ya Sh500,000 na Sh600,000 kutoka mashindano ya Beijing.

Mwandishi huyu alipiga mbizi kutafuta Akinyi na Wamwiri wako wapi na wanajihusisha na shughuli gani miaka 12 baadaye. Akinyi, ambaye Machi 10, 2020, alisherehekea kufikisha umri wa miaka 31, bado ni mchezaji, ingawa pia amejitosa katika kufundisha makinda mchezo wa taekwondo katika shule na mitaani mjini Mombasa.

“Najihusisha pia na kufunza watoto fani za duathlon (inayojumuisha mbio za miguu na zile za baiskeli) na triathlon (inajumuisha uogeleaji, kuendesha baiskeli na kutimka mbio),” anasema Milka kabla ya kufafanua kuwa hajihusishi na masuala ya uogeleaji.

Afisa mmoja kutoka Shirikisho la Taekwondo Kenya alieleza Taifa Leo kuwa Milka angekuwa bado mkali katika timu ya taifa ya taekwondo, lakini yeye huonekana tu wakati kuchaguliwa kwa timu ya taifa. Hata hivyo, Milka alielekeza kidole cha lawama kwa KTF akisema kuwa shirikisho hilo linavunja wachezaji moyo.

“Wachezaji wengi wazoefu wanapotea kwa sababu ya kuvunjwa moyo. Wakati wa kuchaguliwa kwa timu ya taifa, utapata umefanya vizuri, lakini hauko kikosini. Pia, KTF inaepuka kuchagua wachezaji wazoefu kwa sababu wanafahamu haki zao. Wachezaji wazoefu wakikataa kufanya jambo fulani wanaambiwa kuwa wamekosa nidhamu. Pia, timu inapochaguliwa utasikia kuwa hauko kikosini kwa sababu wewe ni mzee. Wameamua zaidi kuchagua timu ya taifa inayojumuisha machipukizi kwa sababu wengi hawajui haki zao,” anadai.

Milka alikuwa katika michezo ya Bara Afrika (African Games) nchini Morocco mwaka 2019 alikovuna zaidi ya Sh200,000 kuwa katika timu ya taifa. Hata hivyo, anasema imekuwa vigumu kuwekeza tuzo za kuwakilisha taifa kimataifa kwa sababu ya majukumu mengi.

“Nina watoto watatu, ambao nawalea pekee yangu. Mmoja ana anemia na wakati mwingine unapopata fedha baada ya kuwakilisha taifa, unapata zinaenda katika matibabu na mahitaji mengine,” anasema Milka, ambaye amekiri kuwa ameathirika vibaya kimapato kutokana na janga la virusi vya corona kwa sababu wazazi sasa hawaruhusi watoto kufanyishwa mazoezi.

Kujihusisha kwake katika uchezaji wa taekwondo kwa bahati nzuri kumemweka katika mstari wa mbele kupokea msaada wa kifedha kutoka kwa serikali wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona.

“Milka yuko katika orodha ya wachezaji 22 na maafisa 22 ambao shirikisho la KTF liliwasilisha kwa Wizara ya Michezo wapate kusaidiwa kutokana na kuwa yeye ni mchezaji wa timu ya taifa na pia hutegemea taekwondo kupata riziki yake ya kila siku,” alisema Katibu Mkuu wa shirikisho hilo George Wasonga.

Wamwiri hatajiriwi kunufaika na mpango huo wa kusaidiwa na serikali.

“Yeye (Wamwiri) si mchezaji wa taekwondo tena,” alisema Wasonga hapo Alhamisi.

Wamwiri anaendelea kupata afueni baada ya kufanyiwa upasuaji wa kichwa miezi miwili iliyopita.

“Nilikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kufanyiwa upasuaji, lakini sasa niko nyumbani naendelea kupata nafuu,” Wamwiri alisema.

Wamwiri aliambia Taifa Leo kuwa yeye bado ni mchezaji, ingawa naibu wa mwekahazina wa KTF Nesmas Wesonga pia alisema kuwa Wamwiri aliacha kucheza taekwondo miaka kadhaa iliyopita.

Aidha, Wamwiri amepuuzilia mbali ripoti kuwa aligeukia pombe kupindukia baada ya kupoteza kazi yake katika kampuni ya mafuta ya Kenol-Kobil.

“Mimi sijawahi kuwa na tatizo la uraibu wa pombe,” alisema Wamwiri alipoulizwa kama habari hizo zilikuwa za kweli ama porojo.

Baada ya kukosa mwakilishi katika taekwondo kwenye Olimpiki mwaka 2012 jijini London nchini Uingereza na 2016 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil, Kenya ilipata tiketi kupitia michezo ya Afrika mjini Rabat nchini Morocco mwaka 2019.

Faith Ogallo alivuna medali ya fedha kutoka Rabat na kujihakikishia nafasi katika makala yajayo ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2021.

“Nilikuwa mmoja wa makocha waliopatia Ogallo ushauri mjini Rabat. Naamini anaweza kuenda mbali kimchezo. Ana umbo la mchezaji wa taekwondo, ambalo ni kuwa mrefu. Pia, ana nguvu na ameimarika sana kimchezo tangu aonekane mara ya kwanza kimataifa mjini Rabat. Yeye kila mara ni mtu ambaye yuko tayari kujifunza na ni mtulivu. Natumai ustaa ambao ameanza kupata hautamwingia akilini kiasi cha kumpotosha,” alisema Wesonga kuhusu mchezaji huyo, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kibabii katika Kaunti ya Bungoma.

You can share this post!

Real Madrid yaendelea kuongoza kwa utajiri duniani –...

TANZIA: Mwanamuziki John Nzenze aliyevumisha...

adminleo