Wanavikapu wa Kenya Morans sasa watia jicho kwa fainali za Kombe la Dunia
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Cliff Owuor wa timu ya taifa ya wanavikapu wa Morans, amesema Kenya ina nafasi maridhawa zaidi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia iwapo kikosi kitajitahidi zaidi.
Kwa mujibu wa Owuor, Morans watakuwa na kila sababu ya kutinga nusu-fainali za kipute cha mwaka ujao cha FIBA AfroBasket na kujikatia tiketi ya Kombe la Dunia mnamo 2023 iwapo watapigwa jeki vya kutosha.
Ni siku nne zimepita tangu vikosi vya taifa vya mchezo wa vikapu kwa upande wa wanaume na wanawake viliandaliwe chakula cha mchana katika hoteli ya Panafric, Nairobi mnamo Agosti 8, 2020.
Dhifa hiyo ilidhaminiwa na mfanyabiashara maarufu Eliud Owalo ambaye pia aliwapa wanavikapu hao kima cha Sh350,000 kadri wanavyozidi kusubiri mwelekeo utakaotolewa na Wizara ya Michezo kuhusu jinsi shughuli za michezo zitakavyorejelewa humu nchini wakati huu wa janga la corona.
“Malengo tuliyojiwekea ni makubwa. Iwapo tutapata msaada wote tunaohitaji na tufanikiwe kushawishi wanavipaku wetu wote mahiri wanaochezea ughaibuni kujumuika nasi kwa kibarua kinachotusubiri, sioni chochote kingine kitakachotuzuia kunogesha Kombe la Dunia,” akasema Owuor.
Kipute cha Vikapu vya Kombe la Dunia kitafanyika nchini Indonesia, Japan na Ufilipino mnamo 2023. Itakuwa mara ya kwanza katika historia kwa mashindano hayo kuandaliwa katika zaidi ya nchi moja.
Kwa Kenya Morans kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za FIBA AfroBasket zitakazoandaliwa jijini Kigali, Rwanda mwaka ujao, itawalazimu mwanzo kuwapepeta miamba wa Afrika Angola, Senegal na Msumbiji katika mechi za kufuzu mnamo Novemba.
Owuor amesema ana mipango kabambe ya kutambisha kikosi chake katika michuano hiyo ya mchujo wa mikondo miwili itakayokamilika mnamo Februari 2021. Kati ya mikakati yake ni kutegemea wanavikapu wanaocheza ughaibuni, wakiwemo Alonzo Ododa na Preston Bungei wanaochezea Amerika na Desmond Owili anayenogesha Ligi Kuu ya Vikapu nchini Australia.
Ododa ni mwanawe mwanavikapu wa zamani wa Kenya, Sebastien Ododa ambaye hadi kuondoka kwake humu nchini na kuyoyomea Amerika, aliwahi kuvalia jezi za Posta na KCB Lions.
“Itanijuzu kuwaangusha miamba wa bara la Afrika ili nami nijitengenezee jina katika ulingo wa vikapu vya kimataifa,” akaongeza Owuor.
Owuor anapania kurejesha kumbukumbu za 1992 ambapo kocha Tom Munyama aliwaongoza wanavikapu wa kike wa Kenya kutwaa nishani ya fedha katika Michezo ya bara Afrika. Mafanikio hayo yaliwapa Kenya tiketi ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia nchini Australia mnamo 1994.
Morans wameratibiwa kufungua kampeni zao za Kundi B za kuwania taji la FIBA Afro-Basket dhidi ya Senegal mnamo Novemba 27. Watapepetana na Angola mnamo Novemba 28 katika mchuano wa pili kabla ya kufunga mechi za makundi kwa kupimana ubabe na Msumbiji mnamo Novemba 29.
Mkondo wa pili ya kipute cha Afro-Basket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021, kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, wanavikapu wa Owour watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.
Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.
Chini ya Owuor, Kenya inalenga kunogesha fainali za AfroBasket kwa mara ya kwanza tangu 1993.