Michezo

Wanawake kutoana jasho Mei 26 Kombe la Afrika raga

April 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga ya Afrika (Rugby Afrique) limetangaza tarehe za Kombe la Afrika la wachezaji saba kila upande la wanawake la mwaka 2018.

Taarifa kutoka shirikisho hilo limesema kwamba kombe hilo litaandaliwa Mei 26 na Mei 27 jijini Gaborone nchini Botswana.

Orodha ya mataifa yanayotarajiwa kushiriki kombe hili inajumuisha Afrika Kusini (mabingwa watetezi), Kenya, Botswana, Uganda, Zimbabwe, Morocco, Tunisia, Senegal, Madagascar na Mauritius.

Afrika Kusini ilizaba Kenya 17-12 katika fainali Septemba mwaka 2017 mjini Tunis nchini Tunisia.

Kombe hili litatumika kuchagua mwakilishi wa Bara Afrika katika makala yajayo ya Michezo ya Olimpiki yatakayofanyika jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Kenya ilipeperusha bendera ya Afrika katika Olimpiki jijini Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka 2016. Ilipata tiketi baada ya Afrika Kusini kujiondoa. Afrika Kusini imepiga Kenya katika fainali nne mfululizo za Afrika.

Jijini Rio, Lionesses ilinyukwa 52-0 na New Zealand, ikalemewa 40-7 na Ufaransa na kupoteza 19-10 dhidi ya Uhispania katika mechi za makundi. Ilipigwa 24-0 na Japan katika mechi za nusu-fainali ya kuorodhesha nambari tisa hadi 12 kabla ya kuzima Colombia 22-10 na kumaliza katika nafasi ya 11.