Wanyama kwenye rada ya West Ham
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA mara tatu wa Kombe la FA West Ham United wanamezea mate nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama, tetesi nchini Uingereza zinadai.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, mabingwa hao wa FA mwaka 1964, 1975 na 1980 watakimbilia kiungo huyu wa Tottenham Hotspur mwenye umri wa miaka 28 iwapo mzawa wa Uhispania Pedro Obiang atahama London Stadium katika kipindi hiki cha uhamisho.
West Ham inatarajia kupoteza kiungo huyu wa Equatorial Guinea mwenye umri wa miaka 27 anayeaminika yumo mbioni kujiunga na Sassuolo nchini Italia kwa Sh1.2 bilioni.
Inasemekana kuwa uhamisho wa Obiang ukifaulu, kocha Manuel Pellegrini kutoka Chile atamakinika zaidi kuimarisha safu ya kati na inaaminika Wanyama huenda akaajiriwa kuwa suluhu katika nafasi hiyo.
Kufuatia Spurs kuvunja benki kununua kiungo Mfaransa Tanguy Ndombele kwa Sh6.9 bilioni mnamo Julai 2, Wanyama anatarajiwa kutumiwa kwa uchache sana na kocha Mauricio Pochettino.
Idadi ya mechi
Mkenya huyu, ambaye anakaribia kupata uraia wa Uingereza pia, amechezea Spurs jumla ya mechi 46 pekee katika misimu miwili iliyopita ya 2017-2018 na 2018-2019 kutokana na kusumbuliwa na majeraha na pia ushindani mkali kikosini na kumlazimika kuchangia padogo timuni.
Alikuwa na mchango mkubwa msimu wake wa kwanza 2016-2017 alipowasili kutoka Southampton na kuchezea Spurs mechi 47.
Huenda uhamisho ukamfaa Wanyama na pia ukawa wa busara kwa West Ham kujaza nafasi ya Obiang inapolenga kupiga hatua mbele kutoka kwa nafasi ya 10 ambayo ilimaliza msimu 2018-2019.