Wanyonyi avuna Sh12.9 milioni kutoka Grand Slam Track nchini Jamaica
BINGWA wa Olimpiki mbio za mita 800, Emmanuel Wanyonyi ameongeza Sh12.9 milioni (Dola za Amerika 100,000) kwenye akaunti yake baada ya kuibuka mshindi wa mbio za 800m/1,500m kwenye mashindano ya Grand Slam Track mjini Kingston, Jamaica yaliyofanyika Aprili 4-6, 2025.
Wanyonyi alimaliza 1,500m katika nafasi ya kwanza na nambari mbili katika 800m.
Katika 1,500m, Wanyonyi alibwaga majina makubwa – bingwa wa Olimpiki Cole Hocker, bingwa wa dunia Josh Kerr na mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki Yared Naguse.
Wanyonyi alishinda 1,500m kwa dakika 3:35.18 akifuatiwa na Waamerika Nuguse (3:35.36) na Hocker (3:35.52), Waingereza Neil Gourley (3:35.60) na Kerr (3:35.61) na nyota wa Canada, Marco Arop (3:39.65).
Katika 800m, Arop alikamata nafasi ya kwanza kwa 1:45.13 akifuatiwa na Wanyonyi (1:46.44) na Mwamerika Bryce Hoppel (1:47.02), mtawalia.
Matokeo yote ya 800m na 1,500m yalipojumuishwa, Wanyonyi alimaliza katika nafasi ya kwanza kwa alama 20 akifuatiwa na Arop (15), Nuguse (11) na Hocker (10), mtawalia.
Ronald Kwemoi alizawadiwa Sh2.6m kwa kumaliza mashindano hayo katika nafasi ya tano kwa jumla katika kitengo cha 3,000m/5,000m.
Kwemoi alikamilisha 3,000m katika nafasi ya nne kwa 8:04.12, nyuma ya Waethiopia Hagos Gebrhiwet (7:51.55) na Telahun Bekele (8:00.68) na Mwamerika Grant Fisher (8:03.85).
Mkenya huyo aliridhika na nafasi ya tano katika 5,000m kwa 14:40.64, nyuma ya Waamerika Fisher (14:39.14), Cooper Teare (14:39.31) na Dylan Jacobs (14:39.56) na Muethiopia Gebrhiwet (14:40.20).
Mshikilizi wa rekodi za dunia za mbio za barabarani za kilomita tano na kilomita 10 Agnes Ngetich pamoja na Hellen Ekalale waliridhika na Sh6.5 milioni na Sh3.2 milioni katika mbio za 3,000m/5,000m baada ya kuzimaliza katika nafasi ya pili na tano kwa jumla, mtawalia.
Wethiopia Ejgayehu Taye (8:28.42) na Tsigie Gebreselama (8:38.15) walikamata nafasi ya kwanza na tatu katika 3,000m nao Ngetich (8:28.75) na Ekalale (8:42.51) wakawa nambari mbili na nne, mtawalia.
Katika 5,000m, Taye aliibuka mshindi kwa 14:54.88 akifuatiwa na Ngetich (14:59.80), Gebreselama (15:24.62), Mwamerika Emily Infeld (15:26.87) na Ekalale (15:28.70) katika usanjari huo.
Susan Ejore na bingwa wa dunia wa 800m Mary Moraa walikamata nafasi ya tano na nane (mkiani) katika 800m, mtawalia.
Ejore alifanya vyema katika 1,500m ambapo alimaliza nafasi ya pili kwa 4:05.10, nyuma ya Muethiopia Diribe Welteji (4:04.51) naye Moraa hakushiriki.
Ejore alizawadiwa Sh3.9 milioni naye Moraa akatia mfukoni Sh1.3 milioni.
Washindi walituzwa Sh12.9 milioni nao nambari mbili hadi nane Sh6.4 milioni, Sh3.9 milioni, Sh3.2 milioni, Sh2.6 milioni, Sh1.9 milioni, Sh1.6 milioni na Sh1.3 milioni, mtawalia.