Waogeleaji wa Umoja Sharks watawala mashindano ya Kaunti ya Kiambu
UMOJA Sharks SC waliibuka washindi wa jumla kwenye mashindano ya kuogelea ya mwaliko ya Chama cha Uogeleaji cha Kaunti ya Kiambia (KCAA) yaliyofanyika katika shule ya Regis mtaani Runda, Kiambu mnamo Mei 10–11.
Mashindano hayo yalivutia waogeleaji 240 kutoka shule na klabu 19.
Umoja ilizoa jumla ya medali 73 (dhahabu 34, fedha 25, shaba 14). Orca SC ilikamata nafasi ya pili ikiwa na medali 76 (dhahabu 33, fedha 30, shaba 13), huku Aga Khan Academy ikifunga tatu-bora kwa nishani 70 (dhahabu 18, fedha 26, shaba 26).
Katika kitengo cha wasichana, Umoja Sharks waliongoza kwa medali 42 (dhahabu 20, fedha 13, shaba 9), wakifuatiwa na Braeburn SC (dhahabu 8, fedha 9, shaba 7) na Orca SC (dhahabu 8, fedha 5, shaba 6).
Orca SC ilimaliza juu ya msimamo wa medali kwa upande wa wavulana ikiwa na 57 (dhahabu 27, fedha 23, shaba 7), ikifuatiwa na Aga Khan Academy (dhahabu 12, fedha 11, shaba 13) na Umoja Sharks (dhahabu 12, fedha 10, shaba 5).
Miongoni mwa waliosisimua mashabiki vilivyo ni Stephanie Wambui,13, kutoka Orca, aliyetawala mbio za mita 100 Freestyle kwa dakika 1:17.45.
Maxwell Kamau, 10, kutoka Woodcreek School, alitwaa ushindi wa 100m Freestyle kwa wavulana kwa 1:43.82, akisema alijitahidi mazoezini kwa sababu alitarajia ushindani mkali.
Makena Waweru kutoka Jawabu School na Ezra Muhia kutoka Beapro SC walisifu mashindano hayo kwa kutoa jukwaa la kukuza vipaji. Muhia alifichua kuwa matumaini yake sasa ni kuwakilisha Kenya kwenye mashindano ya dunia ya kuogelea siku moja.
Kocha Adrian Akath kutoka Kigwa Ridge alisifu mapokezi mazuri, akisema ilikuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki katika mashindano hayo. Mzazi Paul Bokot alisisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kulea talanta zinazoinuka.
Katibu Mkuu wa KCAA, Douglas Okatso, aliridhika na kujitokeza kwa wingi kwa washiriki na kutaka serikali ya Kaunti ya Kiambu kutoa usaidizi zaidi kwa michezo ya kuogelea.
Mashindano hayo yalitumika kama mchujo wa Mashindano ya Kitaifa yatakayoandaliwa na Shirikisho la Uogeleaji Kenya (Kenya Aquatics) hapo Mei 31 katika bwawa la kimataifa la Moi, Kasarani.