Wataalamu watua nchini kusaidia maandalizi ya Kip Keino Classic
Na GEOFFREY ANENE
WATAALAMU kutoka kampuni ya kuandaa michezo ya Golazo waliwasili Kenya mnamo Jumatano kutoka Ubelgiji kusaidia wenyeji katika maandalizi ya makala ya kwanza ya riadha za Kip Keino Classic zitakazofanyika uwanjani Nyayo mjini Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020.
Duru ya Kip Keino ni ya mwisho kwenye Riadha za Dunia za Continental Tour baada ya Paavo Nurmi Games (Turku, Finland), Gylai Istvan Memorial (Szekesfehervar, Hungary), Kawasaki Golden Grand Prix (Tokyo, Japan), Kamila Skolimowska Memorial (Chorzow, Poland), Ostrava Golden Spike (Czech) na Hanzekovic Memorial (Zagreb, Croatia). Nanjing (Uchina), FBK Games (Hengelo, Uholanzi) na Racers Adidas Grand Prix (Kingston, Jamaica) zilifutiliwa mbali kutokana na janga la virusi vya corona.
Kenya ilirejelea riadha yake majuzi tu baada ya michezo yote kusitishwa ghafla mwezi Machi kisa cha kwanza cha virusi hivyo hatari kilipothibitishwa.
Wakati wa kuzinduliwa rasmi kwa Kip Keino Classic hapo Septemba 21, Waziri wa Michezo Amina Mohamed alitangaza kuwa mashabiki 6,000 wataruhusiwa uwanjani Nyayo. Uwanja huo ulifunguliwa na Rais Uhuru Kenyatta hapo Septemba 25 baada ya kufanyiwa ukarabati tangu Agosti 2017.
Baadhi ya majina makubwa yaliyotoa ithibati ya kuwania mataji katika vitengo mbalimbali vya Kip Keino Classic ni bingwa wa dunia Beatrice Chepkoech, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, mzawa wa Kenya ambaye ni bingwa wa Bara Asia Winfred Yavi (Bahrain), mshikilizi wa rekodi ya Australia Genevieve Gregson na bingwa wa dunia 2015 Hyvin Kiyeng’. Watatu hawa pamoja na wakimbiaji watashiriki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Bingwa wa mbio za mita 5,000 wa mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2014 Mercy Cherono atarejea ulingoni baada ya kuwa nje miaka miwili. Cherono alikuwa akisumbuliwa na majeraha yaliyomweka mkekani, lakini sasa yuko tayari. Ametangaza atawania taji la mbio za mita 1,500.
Wakenya wanaotesa zaidi wakati huu katika mbio za mita 800 za wanaume Ferguson Rotich, Collins Kipruto na Wycliffe Kinyamal pamoja na bingwa wa Australia Joseph Deng aliyezaliwa katika kambi za wakimbizi ya Kakuma katika Kaunti ya Turkana, wako katika orodha ya wakimbiaji watakaowania taji kwenye kitengo hicho cha mizunguko miwili.
Mabingwa wa dunia Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na maji wanaume), Hellen Obiri (mita 5,000) na Timothy Cheruiyot (mita 1,500) pia watatifua mbele ya mashabiki wa nyumbani uwanjani Nyayo.
Mnamo Septemba 28, Rais wa Shirikisho la Riadha Kenya Jackson Tuwei alithibitisha kuwa rekodi yoyote itakayowekwa wakati wa Kip Keino Classic itatambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani.