Michezo

WATAWAHI? Arsenal kukabili Valencia baada ya kuilaza Napoli

April 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

BAADA ya kuandikisha ushindi wa 1-0 ugenini ugani San Paolo na kufuzu kwa nusu-fainali ya michuano ya Europa League kwa jumla ya mabao 3-0, Arsenal wamepangiwa kupepetana na Valencia ya Uhispania katika mikondo miwili kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali.

Mkwaju wa adhabu wa Alexandre Lacazette katika kipindi cha kwanza uliipatia nafasi Arsenal na kuiwezesha kusonga mbele, baada ya ushindi wa awali wa mabao 2-0 katika mkondo wa kwanza iliyochezewa Emirates.

Wenyeji, Napoli walifanya kila kitu, ikiwa pamoja na kuwaruhusu mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani mapema saa tatu kabla ya mchezo kuanza kwa ajili ya kuongeza morali ya wachezaji wao, lakini hawakufaulu katika juhudi zao.

Mara nyingi, mashabiki hao walionekana kulowa muda ulivyozidi kuyoyoma, wakati vijana wa Unai Emery wakiongoza huku kipa mkongwe Petr Cech akifanya kazi ya ziada kuokoa makombora mara kwa mara.

Kwenye mechi hiyo, nusura Arkadiusz Milik afufue matumaini ya Napoli baada ya kufunga bao ambalo lilikataliwa kwa madai alikuwa ameotea.

Kiungo mahiri, Aaron Ramsey alitolewa mapema kwenye mechi hiyo baada ya kupata majeraha ambayo kwa mujibu wa kocha Emery, huenda staa huyo akakaa nje kwa wiki kadhaa.

Kulingana na kocha huyo, Ramsey aliumia misuli, na kawaida majeraha ya aina hii humfanya mchezaji kukaa nje kwa majuma kadhaa.

Wakati huo huo, wanasoka wa kulipwa wanaosakata katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Wales waligoma Ijumaa kutumia mitandao wa kijamii kwa saa 24 kulalamikia jinsi mitandao hiyo na wasimamizi wa soka wanavyoshughulikia suala la ubaguzi wa rangi.

Hii ni kufuatia visa kadhaa vya ubaguzi dhidi ya wachezaji wenzao katika mechi za karibuni za kimataifa.

Kwenye visa hivyo, nahodha wa Manchester United, Ashley Young alishambuliwa katika mtandao wa Twitter hali ambayo ilimfanya mchezaji wa Watford, Matthew Deeney kuingilia.

Fursa

Deeney alisema kwamba hawatakubali vitendo hivyo kuendelea katika ulimwengu wa soka, huku akiongeza mgomo wa Ijumaa ulinuia kutoa fursa kwa wachezaji kwa sauti moja dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Young pia alitukanwa baada ya United kuondolewa na Barcelona katika kinyang’anyiro cha kuwania kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mapema juma hili.

Katika kisa kingine, Danny Rose wa timu ya taifa ya Uingereza alizomewa wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Euro 2020 nchini Montengro mnamo Machi 2019.

Baadaye, mlinzi huyo wa klabu ya Tottenham Hotspurs alisema hataendelea kuvumilia dhuluma za aina hiyo tena.

Beki wa United, Chris Smalling pia alishutumu kisa hicho huku akisema: “Muda umewadia kwa mitandao ya kijamii kutafakari jinsi ya kukabiliana na suala la ubaguzi wa rangi.”

Kadhalika nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alisema ipo haja ya wamiliki wa mitandao hiyo kuzingatia umuhimu wa kulinda afya ya akili ya watumiaji wa mitandao hiyo bila kujali umri wao, rangi ya ngozi yao, jinsia wala viwango vyao vya mapato.

Chama cha Wanasoka wa Kulipwa nchini Uingereza (PFA) kimesema mgomo wa jana ni mwanzo wa kampeni ya kukabiliana na “ubaguzi wa rangi katika mchezo wa kandanda.”