Michezo

Watford kumwajiri kocha wa zamani wa Maccabi Tel Aviv kuwa kizibo cha Pearson

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD wanatazamiwa kumpokeza Vladimir Ivic mikoba yao ya ukocha ili awe kizibo cha mkufunzi Nigel Pearson aliyefurushwa mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Pearson alitimuliwa uwanjani Vicarage Road zikiwa zimesalia mechi mbili pekee kwa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukamilika rasmi.

Licha ya kupigwa kalamu wakati ambapo Watford walikuwa wakipigania nafasi finyu ya kusalia ligini kwa kampeni za msimu ujao, kikosi hicho kiliteremshwa ngazi hatimaye baada ya kupoteza mechi zote mbili chini ya kocha Hayden Mullins na hatimaye kushushwa daraja.

Serb Ivic, 43, kwa sasa yuko huru baada ya kuwaongoza Maccabi Tel Aviv ya Israel kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu.

Awali, alikuwa amedhibiti pia mikoba ya kikosi cha PAOK.

Ivic hana tajriba yoyote katika soka ya Uingereza ama akiwa mchezaji au kocha japo amewaridhisha pakubwa vinara wa Watford wanaosaka kwa sasa mkufunzi mpya.

Ujio wake ugani Vicarage Road kutamfanya kocha wa nne wa Watford katika kipindi cha miezi 12 baada ya kutimuliwa kwa Javi Gracia na Quique Sanchez Flores mwanzoni mwa msimu huu na kuondoka kwao kukampisha Pearson mnamo Disemba 2019.