Watford wampa Xisco Munoz mikoba yao ya ukocha
Na MASHIRIKA
WATFORD wamemteua Xisco Munoz, 40, kuwa kocha wao mpya baada ya kumfuta kazi Vladimir Ivic.
Munoz ambaye ni raia wa Uhispania anakubali mikoba ya kuwatia makali vijana wa Watford baada ya kuagana na kikosi cha Dinamo Tbilisi cha Georgia.
Mwanasoka huyo wa zamani wa Valencia, Levante na Real Betis anakuwa kocha wa tano kuwafunza Watford chini ya kipindi cha mwaka mmoja.
Ivic alifutwa kazi mnamo Disemba 19, 2020 Watford wakiwa katika nafasi ya tani kwenye msimamo wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship).
Ni pengo la alama nne ndilo lilikuwa likitamalaki kati ya Watford almaarufu ‘The Hornets’ na nambari mbili Bournemouth. Norwich City wanadhibiti kilele cha jedwali kwa alama tisa zaidi kuliko Watford.
Ivic, 43, alifurushwa kambini mwa Watford licha ya kocha huyo raia wa Serbia kutia saini mkataba wa mwaka mmoja kuanzia Agosti 2020 kambini mwa Watford ambao uwanja wao wa nyumbani ni Vicarage Road.
Munoz atasaidiwa kazi uwanjani Vicarage Road na Roberto Cuesta na Jorge Abella ambao sasa wameteuliwa kuwa kocha msaidia na mkufunzi wa viungo vya mwili mtawalia.
Antonello Brambilla, aliyekuwa katika benchi ya kiufundi iliyoongozwa na Ivic, atasalia kambini mwa Watford kuwa kocha wa makipa.