Michezo

Weledi wa Mwalala utaifaa Bandari ligini – Obungu

July 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA Mnyakaji wa Klabu ya Bandari FC Wilson Obungu ambaye sasa ni moja wa wakufunzi katika timu hiyo amesema ujio wa kocha Benard Mwalala utaisaidia sana Bandari kutamba ligini.

Malala aliyechukua nafasi ya Ken Odhiambo ambaye alijiuzulu ili kuendeleza masomo yake ya ukufunzi aliwaongoza Bandari kuwakalifisha Kakamega Homeboyz mabao 2-0 Tarehe 7 Jumamosi mechi iliyosakatwa katika uwanja wa Manispaa ya Mombasa.

“Kocha Ken Odhiambo alikuwa nasi kwa kipindi cha miaka minne na kujiuzulu kwake ilikuwa pigo kubwa kwetu. Hata hivyo alishirikishwa vilivyo kwenye uteuzi wa kocha mpya na hali hiyo imesaidia kurahisisha mabadiliko akilini wachezaji. Tutampa Malala sapoti ili kazi nzuri aliyoianzisha Nzoia FC iweze kutimia hapa Bandari FC,” akasema Obungu.

Aidha mwanadimba huyo alifichua kwamba mbinu mpya za ukufunzi zilizoanzishwa na kocha Malala zimekumbatiwa sana na wanadimba wengine chipukizi na kuzua ushindani mkubwa katika uwaniaji wa  nafasi za kuwajibikia timu.

Bandari walijishughulisha sana katika majira ya soko ya ununuzi wa wachezaji baada ya kuwaleta wachezaji wanne kikosini na kurasimisha dili ya mchezaji Bernard Odhiambo kutoka Gor Mahia aliyekuwa akiwachezea kwa mkopo.

Wanne hao ni Yema Mwana, Benjamin Mosha, Abdallah Riziki kutoka SoNy Sugar na Chipukizi Joseph Lokale kutoka Rain Forest FC.

Bandari FC wana mechi ngumu Jumamosi 14 Julai,2018 dhidi ya kikosi cha vijana wa Rodoflo Zapata, AFC Leopards uwanjani Kenyatta Kaunti ya Machakos.

Obungu amedai kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu ingawa akaeleza matumaini yao ya kutwaa ushindi.

“Mechi dhidi ya AFC Leopards huwa ngumu ila tunajitayarisha kupata ushindi kwa kuwa rekodi yetu ugenini ni ya kupigiwa mfano msimu huu,” akasema Obungu.

Mechi hiyo imeratibishwa kuanza saa kumi jioni siku hiyo.