Michezo

Wenger asema Arsenal wana uwezo wa asilimia 50 kushinda Bayern

April 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA

LICHA ya kupewa nafasi ndogo ya kushinda Bayern Munich Jumatano na kusonga mbele katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA), kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini timu hiyo inaweza kushinda mechi hiyo ya marudiano, ugani Allianz Arena.

“Kila timu ina asilimia 50 kushinda mechi ya marudiano kati ya Bayern Munich na Arsenal na kufuzu kwa nusu-fainali,” alisema kocha huyo mkongwe raia wa Ufaransa.

Zilipokutana katika mkondo wa kwanza ugani Emirates, timu hizo zilitoka sare 2-2, lakini Wenger anaamini uzoefu wa baadhi ya mastaa wa Arsenal unaweza kuwasaidia ugenini.

Wakati timu hizo zikikutana leo usiku, Manchester City wataalika Real Madrid katika mechi nyingine ya marudiano ugani Etihad, Uingereza baada ya timu hizo kuagana kwa 3-3 katika mkondo wa kwanza ugani Santiago Bernabeu.

Arsenal itakosa tu huduma za Jurrien Timber

Arsenal itakuwa na mastaa wao wa uzoefu wakiwemo kipa David Raya, Rice, Jorginho, Thomas Partey, Bukayo Saka, Takehiro Tomiyasu, Gabriel Martinelli, William Saliba, Ben White, lakini itakosa huduma za Jurrien Timber.

Munich watakuwa bila Serge Gnabry aliyeumia katika mkondo wa kwanza, Kingsley Coman, na Alphonse Davies aliyepigwa marufuku, hali inayofanya mambo kuonekana magumu kwa Munich.

Akizungumza baada ya mazoezi ya mwisho mjini Munich, kocha Mikel Arteta alisema timu yake iko tayari kufanya maajabu makubwa.

“Tumeona timu nyingi zikibadilisha matokeo ya awali na kusonga mbele katika mashindano mbali mbali. Ni matumiani kuwa tutaimarika na kushangaza kila mtu leo usiku,” alisema.

“Ndio tuna majeruhi lakini tumepanga kikosi kizuri kilichojaa motisha. Tutajaribu kuzuia tusifungwe. Lakini kocha amewaonya wachezaji wake wasitarajie mteremko. Tunapaswa kuwa waangalifu. Hata kama tutatangulia kufunga mapema,” alisema.

Arsenal wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wakati Bayern wakifurahia nafasi hiyo kwenye Ligi Kuu ya Bundesliga ambayo tayari imenyakuliwa na Bayer 04 Leverkusen, ikiwa imebakisha mechi tano kutamatisha msimu huu.

Bayern wana jina kubwa barani Ulaya baada ya kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa mara sita, lakini Wenger amesema kikosi chao cha sasa kinasuasua chini ya Thomas Tuchel.

Kwa mara ya kwanza tangu 2011, Bayern Munich wameshindwa kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu huu, na wamekuwa wakipata matokeo ya kuchanganya. Walishindwa na Dortmund katika mechi muhimu kwa hivyo hawatakuwa na asilimia 100 leo usiku.

Arsenal wanaingia uwanjani baada ya mwishoni mwa wiki kuchapwa 2-0 na Aston Villa katika mechi ya EPL.

Maono ya Wenger yameungwa mkono na kiungo mshambuliaji Leandro Trossard aliyesema kila mchezaji kikosini anataka ushindi.

“Kila mtu yuko tayari, huenda tukashangaza wengi. Ni fursa kubwa kwa kila mtu, ikikumbukwa ni mashindano ya hadhi kuu duniani.”

RATIBA

Bayern Munich vs Arsenal (10pm, Allianz Arena, Ujerumani),

Manchester City vs Real Madrid (1pm, Etihad, Uingereza)