Wenger asema atarejea kutembea Arsenal 'siku moja'
Na MASHIRIKA
KOCHA wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema yuko tayari kurejea ugani Emirates kutembea ‘siku moja’ kwa sababu hajawahi kurudi uwanjani humo tangu aondoke miaka miwili iliyopita.
Wenger, 70, aliagana na Arsenal mnamo Mei 2018 baada ya kusaidia kikosi hicho cha Uingereza kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu (EPL) na makombe saba ya FA katika kipindi cha miaka 22 ya ukufunzi wake.
Katika mahojiano yake na gazeti la ‘The Times’, Wenger alifichua kwamba wasimamizi wa Arsenal wamekuwa wakimwalika ugani Emirates mara kwa mara, ila msimamo wake umekuwa ni kufuatilia kwa mbali mengi ya matukio yanayoendelea kambini mwa kikosi hicho ambacho kimenolewa na makocha wawili tangu kuondoka wake.
Mrithi wa Wenger, Unai Emery ambaye kwa sasa anawatia makali vijana wa Villarreal nchini Uhispania, alitimuliwa na Arsenal mwishoni mwa 2019 na nafasi yake kutwaliwa na mwanasoka wa zamani wa kikosi hicho, Mikel Arteta.
Wenger amesema kwamba maamuzi ya kuondoka kwake Arsenal yalikuwa magumu na machungu na alizoea hali baada ya muda na kwa sasa hana uhusiano wowote wa karibu na kikosi hicho.
Kinyume na Wenger, kocha Alex Ferguson wa Manchester United, alipokezwa majukumu ya kuwa mwanachama wa Bodi ya Usimamizi ugani Old Trafford baada ya kustaafu ukocha akidhibiti mikoba ya kikosi hicho mnamo 2013.
Mnamo 2019, Wenger alifichua maazimio ya kurejelea ukocha ila akaajiriwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa mkuu wa maendeleo ya soka kimataifa mnamo Novemba 2019.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO