Michezo

Werner afunga mabao mawili katika mechi yake ya mwisho akiichezea RB Leipzig

June 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI Timo Werner alifunga mabao mawili katika mchuano wake wa mwisho wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) akivalia jezi za RB Leipzig na kuhakikisha kwamba anakuwa mfungaji bora wa muda wote wa kikosi hicho kabla ya kuondoka.

Werner mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa sasa kutua jijini London, Uingereza na kuanza kuvalia jezi za Chelsea mnamo Julai 2020 baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Leipzig kwa kima cha Sh7.5 bilioni.

Magoli yaliyofumwa wavuni na Werner yalichangia ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Augsburg ugenini na hivyo kuhakikisha kwamba Leipzig wanakamilisha kampeni za Bundesliga msimu huu katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 66, moja mbele ya Borussia Monchengladbach.

Mabingwa wa msimu huu, Bayern Munich walivuna ushindi wa 4-0 dhidi ya Wolfsburg huku nambari mbili Borussia Dortmund wakisajili pia ushindi sawa na huo dhidi ya Hoffenheim.

Mabao ya Werner yalifikisha idadi yake ya magoli kambini mwa Leipzig hadi 95 kutokana na jumla ya mechi 159.

Magoli 28 ambayo yamefungwa na nyota huyo mzawa wa Ujerumani katika kampeni za Bundesliga muhula huu yanamweka katika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora, nyuma ya Robert Lewandowski wa Bayern ambaye ametikisa nyavu za wapinzani mara 34 msimu huu.

Kati ya mabao yote yaliyofungwa na Werner msimu huu, 17 yalitokana na mechi za ugenini za Leipzig. Idadi hiyo ya magoli ilifikia rekodi ya awali ya mwanasoka Jupp Heynckes aliyewahi kufunga mabao mengi zaidi ya ugenini katika kipindi cha msimu mmoja akivalia jezi za Monchengladbach kati ya 1973-74.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Juni 27):

Dortmund 0-4 Hoffenheim

Augsburg 1-2 RB Leipzig

Wolfsburg 0-4 Bayern Munich

Union Berlin 3-0 Dusseldorf

Leverkusen 1-0 Mainz

M’gladbach 2-1 Hertha Berlin

Frankfurt 3-2 Paderborn

Freiburg 4-0 Schalke

Bremen 6-1 Cologne