Michezo

Werner afunga penalti mbili na kuongoza Chelsea kuadhibu Rennes ya Ufaransa katika soka ya UEFA

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MASOGORA wa kocha Frank Lampard, Chelsea, waliendelea kutamba kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kwa kusajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Rennes ya Ufaransa mnamo Novemba 4, 2020.

Ushindi huo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2016-17, uliwasaza katika ulazima wa kuvuna alama tatu pekee kwenye mechi tatu za marudiano ili kufuzu kwa hatua ya mwondoano ya 16-bora kwenye UEFA msimu huu.

Chelsea walioingia mechini wakijivunia ari ya kuambulia sare tasa dhidi ya Sevilla kabla ya kupiga Krasnodar walichuma nafuu kutokana na wingi wa visa vya majeraha kambini mwa Rennes waliokamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 uwanjani kabla ya mwisho wa kipindi cha kwanza.

Sajili mpya Timo Werner aliwafungia Chelsea mabao mawili kupitia penalti za dakika ya 10 na 41 kabla ya chipukizi Tammy Abraham kufanya mambo kuwa 3-0 kunako dakika ya 50.

Kiungo Chagas Estevao wa Rennes alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 40 baada ya kuonywa mara mbili mechini.

Chelsea walikosa huduma za mwanasoka Kai Havertz katika mechi hiyo baada ya kuugua Covid-19. Mchuano huo ulimpa kipa mpya wa Chelsea, Edourad Mendy jukwaa la kucheza dhidi ya waajiri wake wa zamani waliomwachilia mwanzoni mwa kampeni za msimu huu.

Chelsea kwa sasa wanajivunia kusajili ushindi kutokana na mechi nne kati ya tano zilizopita dhidi ya wapinzani kutoka Ufaransa kwenye UEFA.

Kwa upande wao, Rennes wamepoteza mechi zote tatu za soka ya bara Ulaya dhidi ya wapinzani kutoka Uingereza ambao wamewapokeza kichapo cha jumla ya mabao 7-0.

Jesus Navas wa Sevilla naye alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyowashuhudia wakipepeta Krasnodar 3-2 katika mchuano mwingine wa Kundi E mnamo Novemba 4.