West Brom wamteua Sam Allardyce kurithi mikoba waliyompokonya kocha Bilic
Na MASHIRIKA
KIKOSI cha West Bromwich Albion kimeteua kocha Sam Allardyce kuwa mkufunzi wao kwa mkataba wa miezi 18 ijayo.
Allardyce, 66, hajawahi kudhibiti mikoba ya kikosi chochote tangu aagane na Everton mnamo 2018.
Mkufunzi huyo ambaye kwa sasa anamrithi Slaven Bilic aliyefurushwa na West Brom, amewahi pia kudhibiti mikoba ya klabu saba tofauti katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na hakuna kikosi chochote ambacho amewahi kunoa kimewahi kushushwa ngazi.
Allardyce anaungana na West Brom almaarufu ‘Baggies’ pamoja na Sammy Lee ambaye amewahi kuwa msaidizi wake kwa muda mrefu. Anakubali mikoba ya kikosi hicho wakati ambapo kinashikilia nafasi ya 19 kwenye msimamo wa jedwali kwa alama saba pekee kutokna na mechi 13 za ufunguzi wa msimu huu 2020-21.
Allardyce ambaye ni mzawa wa Dudley, alianza kazi ya ukocha akidhibiti mikoba ya West Brom chini ya Brian Talbot mnamo 1989 na mchuano wake wa kwanza akiwa mkufunzi wa kikosi hicho kwa mara ya pili ni dhidi ya Aston Villa mnamo Disemba 20, 2020.
Licha ya kupoteza jumla ya mechi nane kati ya 13 zilizopita, West Brom waliwalazimishia Manchester City sare ya 1-1 katika gozi la EPL mnamo Disemba 15, 2020 uwanjani Etihad.
Mchuano wa pekee ambao kikosi cha West Brom umeshinda ni dhidi ya Sheffield United (1-0) mnamo Novemba 28, 2020.
Allardyce alifutwa kazi na Everton mnamo Mei 2018 baada ya kudhibiti mikoba yao kwa miezi sita. Japo alikubali mikoba ya kikosi wakati kikiwa katika nafasi ya 13, aliwaongoza kujinyanyua na wakamaliza kampeni zao katika nafasi ya nane.
Kabla ya kujiunga na Everton almaarufu ‘Toffees’, Allardyce alikuwa amejiuzulu kambini Crystal Palace baada ya kuwa nao kwa miezi mitano pekee.
Kazi ya kuwatia makali vijana wa Palace ilikuwa ya kwanza kwa Allardyce baada ya kutimuliwa na timu ya taifa ya Uingereza. Kocha huyo amewahi pia kunoa vikosi vya Bolton Wanderers, Newcastle, Blackburn, West Ham na Sunderland.