Michezo

West Ham yapiga breki rekodi ya kutoshindwa kwa Leicester ligini

October 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

WEST Ham United waliendeleza ubabe wao katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwafunga Leicester City 3-0 mnamo Oktoba 4, 2020, uwanjani King Power.

Kichapo hicho kilikomesha rekodi ya kutoshindwa kwa Leicester ya kocha Brendan Rodgers tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Licha ya kocha David Moyes anayeugua Covid-19 kutokuwepo uwanjani kwa minajili ya mchuano huo, vijana wake walijitahidi vilivyo na kusajili ushindi mnono wiki moja baada ya kuwapepeta Wolves 4-0 katika gozi jingine la EPL.

Michail Antonio aliwaweka West Ham kifua mbele baada ya kushirikiana na Aaron Cresswell kunako dakika ya 14. Cresswell alichangia pia bao la pili la West Ham lililojazwa wavuni na Pablo Fornals kabla ya Jarrod Bowen kuchuma nafuu kutokana na masihara ya beki Caglar Soyuncu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Licha ya kutamalaki mchezo na kuonekana kuwazidi wageni wao maarifa katika kila idara, Leicester walishinda kabisa kulenga shabaha langoni pa West Ham.

Japo Leicester walifungiwa na Harvey Barnes mwishoni mwa kipindi cha pili, bao hilo halikuhesabiwa kwa sababu fowadi Jamie Vardy alikuwa ameotea.

Leicester walijibwaga ugani wakitazamiwa kutia kapuni alama zote tatu baada ya kuwatandika Man-City 5-2 katika mchuano wao wa awali.

Leicester walikosa huduma za wanasoka matata Dennis Praet na James Maddison kwenye safu yao ya kati katika mechi hiyo.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Mei 2017 kwa West Ham kusajili ushindi ugenini dhidi ya kikosi kinachoshikilia nafasi ya tatu-bora kwenye jedwali la EPL.

Tangu wakati huo, West Ham wamepoteza jumla ya mechi tisa na kuambulia sare mara moja.

Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa West Ham kusajili ushindi katika mechi mbili za EPL mfululizo huku wapinzani wakishindwa kuwafunga kwa mara ya kwanza tangu Mei 2019.

Kocha Rodgers wa Leicester sasa amepoteza mechi mbili mfululizo katika mashindano yote kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2012 alipokuwa mkufunzi wa Liverpool.