Michezo

Wito EPL irejelewe baada ya wachezaji wote kupimwa corona

April 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wakufunzi wa Ligi Kuu ya Uingereza (LMA), Richard Bevan, ametaka kipute hicho kurejelewa tu baada ya wachezaji wa vikosi vyote 20 vya ligi hiyo kufanyiwa vipimo vya afya ili kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.

Aidha, Bevan amesisitiza haja ya vipimo hivyo kufanywa kuwa vya lazima na vya mara kwa mara miongoni mwa wachezaji, maafisa, wasimamizi na wakufunzi wote katika hospitali za klabu hizo.

“Baada ya vipimo hivyo kufanywa vya lazima kwa maafisa wa afya na wagonjwa kama hali ilivyo kwa sasa, itakuwa vyema iwapo juhudi hizo zitakumbatiwa na washiriki wa EPL,” akasema Bevan ambaye pia amekashifu hatua ya vinara wa hiyo kutaka EPL ikamilike chini ya muda wa siku 56 pindi itakaporejelewa.

Kwa sasa, Ligi Kuu ya EPL na shughuli zote za soka nchini Uingereza zimesitishwa hadi virusi vya corona vitakapodhibitiwa vilivyo duniani kote.

Kwa mujibu wa Bevan, ingekuwa vyema iwapo waendeshaji wa kipute hicho wangeshauriana mara kwa mara na wakufunzi wa klabu husika na ligi nyinginezo za bara Ulaya ili ratiba yao iafikiane na tarehe ya kurejelewa na kukamilika kwa michuano mingineyo ya bara Ulaya ikiwemo Europa League na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kwa pamoja na Aleksander Ceferin ambaye ni Rais wa Soka ya bara Ulaya, Bevan ameshikilia kwamba huenda vipute vya UEFA na Europa League msimu huu vikatupiliwa mbali iwapo virusi vya homa kali ya corona havitakuwa vimedhibitiwa vilivyo kufikia Septemba 2020.

Hata hivyo, wamewapendekezea vinara wengine wa Uefa kuhusu uwezekano wa mechi hizo kusakatwa ndani ya viwanja vitupu badala ya kuzifutilia mbali kabisa.

Vinyang’anyiro vya UEFA na Europa League kwa sasa vimesitishwa pia kwa muda usiojulikana.

“Hatutaweza kurejelea mapambano hayo iwapo hali itasalia kuwa ilivyo kwa sasa kufikia Septemba au Oktoba,” akasema Ceferin katika mahojiano yake na gazeti la ZDF Sportstudio nchini Ujerumani.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa msimu huu mzima kufutuliwa mbali, alisisitiza kwamba: “Iwapo viongozi na washikadau wa mamlaka husika hawatawaruhusu kucheza, basi itakuwa vigumu kwa vipute hivyo vya Uefa kuendelea”.

Vikosi vya Manchester City na Chelsea kutoka Uingereza ndivyo vingalipo katika kivumbi cha UEFA huku Manchester United, Wolves na Rangers kutoka Scotland zikiwa miongoni mwa timu ambazo bado zinawania ufalme wa Europa League muhula huu.

Ceferin amesema kuwa maamuzi zaidi kuhusu mpangilio mpya wa kuahirishwa zaidi, kufutiliwa mbali au kurejelewa kwa mechi hizo yatatolewa baadaye wiki hii na Bodi ya Soka ya Ulaya ambayo imewaalika tena wawakilishi na wajumbe wa mashirikisho yote 55 ya soka duniani kwa mkutano maalum.