Wito kwa serikali, Nike kujenga miundomsingi ya riadha dunia ikimuaga Kiptum
NA HASSAN WANZALA
VIONGOZI mbalimbali wametoa wito kwa serikali na kampuni za vifaa vya michezo kuwajali wanariadha ili kupiga jeki juhudi zao za kuizolea Kenya sifa na medali katika ulingo wa spoti.
Wakiongea Ijumaa wakiwa Chepkorio katika hafla ya ibada kabla ya mazishi ya mshikilizi wa rekodi ya marathon Kelvin Kiptum, viongozi walisema ni wajibu wa serikali na kampuni kama Nike na Golazo kutengeneza miundomsingi eneo pana la North Rift na kuwapa wanariadha vifaa na mazingira mazuri.
Gavana wa Elgeyo Marakwet Wesley Korir alisema marehemu Kiptum alikuwa mtu wa kujitolea katika riadha na hiyo bila shaka ndio ilikuwa sababu ya nyota yake kung’aa katika mbio za masafa marefu.
“Kiptum alikuwa ameahidi kufanya makubwa. Alikuwa ameniambia nihudhurie kutazama mbio za marathon katika mashindano ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa baadaye mwaka huu 2024, nimuone akikimbia mbio hizo kwa muda chini ya saa mbili,” akasema gavana Korir huku akisikitika ndoto ya Kiptum haitatimia.
Gavana huyo alisema serikali ya Kenya Kwanza tangu Septemba 13, 2022, imeleta mageuzi makubwa ambapo hata wanariadha na wanamichezo mengine wakienda kushiriki mashindano nje ya nchi, hawalali tena sakafuni.
Mwenzake wa Uasin Gishu Jonathan Bii aliwataka wawekezaji kumiminika Eldoret akisema “hata wale wanariadha wa Elgeyo Marakwet hupenda kustaafu na kutulia Uasin Gishu”.
“Hata tukitoka hapa baada ya ibada, mazishi yanaenda kufanyika kwa shamba la Cherunya, Naiberi katika Kaunti ya Uasin Gishu,” akasema gavana Bii almaarufu ‘Koti Moja’.
Hata hivyo, gavana Korir alidai kauli ya Koti Moja haina maana kwa sababu “ni ama uzaliwe Elgeyo Marakwet au ufanyie mazoezi Elgeyo Marakwet ndipo ufikie kilele cha fani ya riadha”.
Mbunge wa Kapseret na mwandani wa Rais alimtaka kiongozi wa nchi awe akipata nafasi kusemezana na wanariadha na kuwapa ushauri ili kuhakikisha wanajua namna ya kujisimamia kuepuka madhara ya pesa ujanani.
Mbunge wa Keiyo Kusini David Kimaiyo alimwomboleza marehemu kama rafiki ambaye “tulikuwa tunashirikiana vizuri”.
“Niliita wanariadha kwa afisi yangu tukazungumza. Tuliunda kamati ambapo marehemu Kiptum alikuwa mmoja wa wanachama. Wanariadha walituma ujumbe kwa afisi ya Waziri wa Michezo Ababu Namwamba. Walitaka changamoto zao zishughulikiwe,” akasema Bw Kimaiyo.
Mbunge huyo alirejelea ombi la mrushaji mkuki Julius Yego aliyeomba Rais Ruto kuhakikisha katika eneo hilo la Chepkorio, uwanja wa michezo unajengwa na kupewa jina la marehemu Kiptum.
Akizungumza kwa niaba ya wanariadha, Yego aliomba serikali iwe ikimpa kila mwanariadha-nyota mlinzi na dereva.
“Hatujui kinachoweza kumfanyikia binadamu, lakini pengine Kiptum angekuwa na msaidizi huenda maisha yake yangenusurika,” akasema Yego, ambaye naye alizolea Kenya sifa kwa utupaji mkuki katika Olimpiki za Rio mwaka 2016 alipozoa medali ya fedha kwa kutupa mkuki kwa umbali wa mita 88.24. Mwaka 2011, Yego alinyakua dhahabu yake ya kwanza katika mashindano ya All-Africa Games kwa kurusha mkuki kwa umbali wa mita 78.34.
Mbunge wa Keiyo Kaskazini Adams Korir naye alimpongeza Rais Ruto kwa kutangaza mazishi ya nyota Kiptum kuwa mazishi ya kitaifa.
Aidha, Bw Korir alimsifu Kiongozi wa Nchi kwa kumpigia debe hasimu wake mkuu, kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, ambaye alitangaza wazi kwamba anamezea mate kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nandi, Cynthia Muge alisema bunge litajitolea kikamilifu kuhakikisha wanariadha-nyota wanapata heshima, ulinzi na staha.
“Aidha Rais Ruto tunajionea kwamba mradi wa nyumba nafuu unawezekana. Ingawa nyumba ya Kiptum imekuja katika kipindi cha uombolezaji, ni wazi kwamba nyumba za bei nafuu zitawafaa wengi,” akasema Bi Muge.
Waziri Namwamba aliahidi kwamba maeneo ya North Rift yanaendelea kuimarishwa kwa sababu huko ni kitovu cha wanariadha.
“Bidhaa kubwa ya Kenya kwa dunia ni hawa wanariadha wetu,” alisema Bw Namwamba.
Bw Namwamba pia alisema serikali inashirikiana na benki mbalimbali kutoa ushauri kwa wanariadha na wanaspoti kwa ujumla ili kuelewa namna ya kutumia pesa zao.
Kiptum alifariki pamoja na kocha wake Gervais Hakizimana wa kutoka nchini Rwanda, kufuatia ajali ndani ya gari katika barabara ya Eldoret-Eldama Ravine usiku wa Februari 11 kuamkia Februari 12, 2024.
Kiptum aliyefariki akiwa na umri wa miaka 24, amemuacha mjane Asenath Cheruto na watoto wawili, Caleb,7, na Precious,4.
Kiptum alikuwa mtoto wa pekee wa Mzee Samson Cheruiyot na mama Mary Kangogo.
Alijizolea sifa alipovunja rekodi ya Eliud Kipchoge kwa kukamilisha mbio za Chicago Marathon kwa muda wa saa 2:00:35 mnamo Oktoba 8, 2023.
Kabla ya hapo, Kipchoge alikuwa akishikilia rekodi ya muda wa saa 2:01:09 aliyoweka katika mbio za Berlin Marathon mwaka 2022.