Michezo

Wito Shield Cup isitishwe

June 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MWENYEKITI wa Kariobangi Sharks, Robert Maoga ametaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kufutilia mbali kivumbi cha Shield Cup iwapo serikali itakosa kulegeza masharti yaliyowekwa katika juhudi za kudhibiti ugonjwa wa Covid-19.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongeza au kulegeza kanuni zilizopo za kafyu na zile zinazodhibiti mikusanyiko ya umma na usafiri katika baadhi ya maneneo ya humu nchini.

Kwa mujibu wa Maoga, kauli ya Rais itaamua hatima ya mechi zilizosalia katika kipute cha Shield Cup muhula huu. Kabla ya shughuli zote za michezo kusitishwa humu nchini mnamo Machi 2020, kivumbi cha Shield Cup kilikuwa kimefikia hatua ya 16-bora.

FKF ilitamatisha rasmi kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo Aprili na kutawaza Gor Mahia mabingwa huku ikisaza mapambano ya Shield Cup ambayo humpa mshindi fursa ya kuwakilisha Kenya kwenye Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup).

Ingawa FKF inapania kushuhudia mechi zote za Shield Cup zikisakatwa, Maoga ametaka kinyang’anyiro hicho kufutiliwa mbali hata kama Serikali italegeza masharti yaliyopo.

Wito umetolewa na wadau mbalimbali kukubalia Bandari ambao ni mabingwa watetezi wa Shield Cup kunogesha kampeni za CAF Confederations Cup muhula ujao.

“Hata kama sheria zitalegezwa, sidhani kama tuna uwezo wa kufuata kanuni za afya zilizopendekezwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Isitoshe, hatuna miundo-misingi ya kutuwezesha kutekeleza baadhi ya sheria hizo mpya za afya.”

FKF tayari imewasilisha jina la Gor Mahia kwa vinara wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na mabingwa hao wa KPL watawakilisha Kenya kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).

“Ili kuzuia utata ulioibuliwa na FKF baada ya kuwapa Gor Mahia ubingwa wa KPL msimu huu, itakuwa vyema iwapo kampeni za Shield Cup zitafutiliwa mbali na Kenya kutokuwa na mwakilishi kwenye Kombe la Mashirikisho muhula ujao,” akaongeza Maoga.