• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wito wa usawa wa tuzo kwa wanamichezo wa kike, kiume

Wito wa usawa wa tuzo kwa wanamichezo wa kike, kiume

Na FRIDAH OKACHI

WATETEZI wa haki wamelaumu baadhi ya wanasiasa kwa kufadhili mashindano ya michezo katika maeneo mbalimbali yanayoishia kuwabagua wanamichezo wa kike wanaotoka na tuzo duni ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Msimamizi wa shirika la A Pack a Month Jackline Salianne, amedai kwamba katika fainali za Kombe la Cleoh Malala ambazo kilele chake kilikuwa ni Desemba 2023, wachezaji wa kike hawakuwa na lao.

Mashindano hayo yalifadhiliwa na Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala.

Bi Salianne akiendelea kukosoa, anasikitika kwamba wanasiasa wengi hufadhili michezo ya soko kwenye kaunti mbalimbali bila kushirikisha wasichana vilivyo.

“Kumekuwepo na Kombe la Cleoh Malala ambalo liliendelea kwa muda mrefu. Unapata kuwa washindi wa kiume wanapewa pesa nyingi kuliko wanawake. Wanaumme walikuwa wakipewa Sh500,000 lakini wanawake wakapewa Sh200,000,” alisema Bi Salianne.

Bi Salianne alisema hayo wakati wa mashindano ya mchezo wa soka yaliyowavutia wasichana wa chini ya umri wa miaka 18.

Wasichana wakicheza katika uwanja wa Kasoro Bahari ulioko eneo la Embulbul katika Kaunti ya Kajiado. PICHA | FRIDAH OKACHI

Mechi hizo zilisakatwa katika uwanja wa Kasoro Bahari eneo la Embulbul, Kajiado Kaskazini katika Kaunti ya Kajiado.

Wasichana kutoka timu za Achievers na Matasia Starlets walinufaika pakubwa kwa kuelimishwa kuhusu namna ya kuepuka kupata mimba za mapema na pia masuala kuhusu dhuluma za kijinsia.

Zawadi na tuzo kutoka kwa wadhamini wa michuano ya soka. PICHA | FRIDAH OKACHI

Msichana Grace Naseku, 15, aliambia Taifa Leo kuwa wakati wa mechi hiyo, wengi hupata fursa za ufadhili wa masomo kutoka kwa watazamaji na kujiunga na shule ambazo hawakuwa wanatarajia.

“Binafsi, soka imenisaidia kuonyesha dunia makali ya talanta yangu na kupata ufadhili wa masono. Pia, wakati tunacheza kuna wale wanaotushangilia na kuwa msaada kwetu huku nje. Unapata kuna shule nyingine ambazo hutuchukua na tunanufaika kwa elimu,” alisema Naseku.

Wadau waliokuwepo wakati wa mechi hiyo ya wasichana ni maafisa wa kutoka Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) na Rotary Club.

Bw Benacite K anayefanya kazi katika NCIC, alisema kujiunga na akina dada hao ni njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kwa kuondoa ukabila hasi.

“Hali ni ngumu na tumefika hapa kutoa sodo kwa wasichana wetu na kuondoa ukabila hasi. Tunatumia fursa hii ya mchezo kama njia ya kutatua mizozo na migogoro inayopatikana kwenye jamii,” alisema Bw Benacite K.

  • Tags

You can share this post!

Ruto hajakita mizizi kisawasawa serikalini – Joe Nyutu

Wazazi wajiandaa kuwapeleka watoto shuleni

T L