Wolves waadhibiwa kwa kukiuka kanuni za UEFA
Na CHRIS ADUNGO
WOLVES wataruhusiwa kusajili wachezaji 23 pekee kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao iwapo watafuzu kwa kipute hicho msimu ujao kwa kunyanyua ufalme wa Europa League muhula huu.
Hii ni baada ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukosa kutimiza kanuni za matumizi ya fedha kwa mujibu wa viwango vya Uefa (FFP).
Wolves waliwapepeta Olympiakos mnamo Agosti 6, 2020 na kufuzu kwa robo-fainali za Europa League kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 48.
Kwa kusonga mbele zaidi na hatimaye kutwaa taji la Europa League, Wolves watajikatia tiketi ya kunogesha soka ya UEFA msimu ujao wa 2020-21 na kufanya kivumbi hicho kuwa na wawakilishi watano kutoka Uingereza baada ya Liverpool, Manchester City, Manchester United na Chelsea waliofunga mduara wa nne-bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.
Hata wakifanikiwa kufuzu kwa kivumbi hicho, Wolves watakubaliwa kuunga kikosi cha wanasoka 25 pekee kwenye ‘Orodha A’ ya Uefa, hii ikiwa adhabu kwa kutumia fedha nyingi kupita kiasi kwa minajili ya kufuzu kwa kipute hicho msimu huu.
Wolves kwa sasa wanajiandaa kupepetana na mabingwa mara tano wa Europa League, Sevilla katika gozi litakalowakutanisha mjini Duisburg, Ujerumani mnamo Jumanne ya Agosti 11, 2020.
Kwa mujibu wa Uefa, Wolves walitumia Sh3.7 bilioni za ziada katika kampeni za msimu huu wa 2019-20 tofauti na kiasi cha fedha walizotumia katika misimu ya awali. Hizi ni fedha ambazo kwa sasa wanalazimika kufidia Uefa kufikia mwisho wa kampeni za muhula ujao wa 2020-21.