Wolves wang'ata Sheffield
Na MASHIRIKA
WOLVES walifunga mabao mawili chini ya dakika sita za kipindi cha kwanza na kuanza vyema kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwapokeza Sheffield United kichapo cha 2-0 mnamo Septemba 14, 2020 ugani Bramall Lane.
Vikosi vyote vilishuka dimbani baada ya kujivunia kampeni bora zaidi muhula uliopita ulioshuhudia Sheffield wakiambulia nafasi ya tisa huku Wolves wakiridhika na nafasi ya saba kwenye EPL na kutinga robo-fainali za Europa League.
Hata hivyo, ni masogora wa kocha Nuno Espirito ndio walioanzia mahali walipokamilishia muhula uliopita kwa kufunga mabao mawili ya haraka kupitia kwa Raul Jimenez na Romain Saiss katika dakika za tatu na sita mtawalia. Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa kipa Aaron Ramsdale kudakia Sheffield United.
Sheffield United walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara huku jaribio lao la pekee langoni pa Wolves likija katika dakika ya 38 ila fataki ya Oli McBurnie ikadhibitiwa vilivyo na kipa Rui Patricio.
Ushauri ambao kocha Chris Wilder aliwapa vijana wake wakati wa mapumziko ulionekana kuzalisha matunda mwanzoni mwa kipindi cha pili. Sheffield United walirejea kwa matao ya juu huku John Fleck akishuhudia kombora lake likibusu mhimili wa goli la Wolves naye John Lundstram akikosea kidogo tu kujaza kimiani krosi ya Billy Sharp.
Ramsdale alilazimika kufanya kazi ya ziada kuwanyima Wolves bao la tatu baada ya Saiss, 22, aliyesajiliwa kutoka Bournemouth msimu huu kwa kima cha Sh2.5 bilioni kushuhudia kombora lake likibusu mwamba kabla ya Jimenez kupaisha mpira licha ya kusalia peke yake na golikipa wa Sheffield United.
Wolves walirishisha sana katika mchuano huo licha ya kutojishughulisha vilivyo sokoni mwishoni mwa msimu uliopita ambapo walisakata zaidi ya mechi 60 kati ya Julai 2019 na Agosti 2020.
Sheffield United wanajiandaa kwa sasa kuvaana na Burnley katika raundi ya pili ya Carabao Cup mnamo Septemba 17 huku Wolves wakiwaalika Stoke City siku hiyo hiyo kwa kipute cha Carabao Cup ugani Molineux.
TAFSIRI: CHRIS ADUNGO