Yachukua miaka 49 Southampton kuangusha Burnley katika EPL
Na MASHIRIKA
SOUTHAMPTON walijinyanyua kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuwapiga Burnley kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 49.
Bao la Danny Ings katika dakika ya tano lilitamatisha pia rekodi mbovu ya Southampton kwenye kampeni za hadi kufikia sasa muhula huu.
Baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mnamo Septemba 12, Southampton walibanduliwa na Brentford kwenye raundi ya pili ya Carabao Cup kwa kucharazwa magoli 2-0 mnamo Septemba 16.
Hadi walipowaangusha Burnley, kikosi hicho cha kocha Ralph Hasenhuttl kilikuwa kimetandikwa 5-2 na Tottenham Hotspur mnamo Septemba 20 uwanjani St Mary’s.
Bao lililofungwa na Ings lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Che Adams na sajili mpya Kyle Walker-Peters.
Burnley waliokosa wachezaji saba wa kikosi cha kwanza kutokana na majeraha, walilalamikia baadhi ya maamuzi ya refa Andre Marriner wakidai penalti baada ya fowadi Chris Wood kuangusha mara mbili na Jan Bednarek ndani ya kijisanduku.
Wood nusura asawazishe mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili ila jitihada zake zikazimwa na kipa Alex McCarthy ambaye pia aliwanyima Charlie Taylor na Ashley Westwood nafasi tatu za wazi.
Southampton waliwapiga Burnley kwa mara ya mwisho katika gozi la EPL mnamo Machi 1971.