Yaibuka mashabiki wa #MashemejiDerby waliharibu mali ya Sh3m Kasarani
NA CECIL ODONGO
KIWANGO cha uharibifu kilichosababishwa na mashabiki uwanjani MISC Kasarani wakati wa debi ya Mashemeji Jumamosi Agosti 25 inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh 3 milioni.
Mashabiki wa AFC Leopards walivunja viti uwanjani humo wakilalamikia uamuzi wa refa katika mechi hiyo iliyowakutanisha na mahasimu wao wa tangu jadi Gor Mahia.
K’Ogalo waliishia kushinda mtanange huo kwa mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa KPL kwa mara ya 17 na mwaka wa pili mfululizo zikiwa bado zimesalia mechi 6 ligi hiyo ikamilike.
Kutokana na vurugu hizo, bodi simamizi ya viwanja nchini imewapiga Ingwe marufuku dhidi ya kutumia uwanja huo na pia huenda mabingwa hao mara 13 wa KPL wakagharamika zaidi kulipia uharibifu huo kutoka kwa pesa za hazina ya klabu.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Sports Kenya Saima Ondimu, zaidi ya viti 1000 vilivunjwa na ukaguzi zaidi unaendelea kufanyiwa kabla ya AFC Leopards kuangushiwa adhabu kubwa ya kugharimia uharibifu huo.
“Tathamini ya mwanzo mwanzo inaonyesha kwamba zaidi ya viti 1000 viling’olewa na kutupwa uwanjani na mashabiki wa AFC Leopards. Mwaka jana gharama ya kila kiti ilikuwa Sh 2,500 na kiwango hicho huenda kimepanda. Tutafanya tathmini za mwisho Jumatatu Agosti 27 ili kujua kiwango cha uharibifu kisha tuwasilishie na wawajibikie,” akasema Bi Ondimu.
Uwanja huo ulifunguliwa majuzi baada ya miezi kadhaa ya ukarabati wake na haujakuwa ukitumiwa kwa mechi za KPL ingawa umeandaa mechi za kuwania ubingwa wa kombe la Mashirikisho barani Afrika CAF unaohusisha Gor Mahia.
Wakati uo huo wakufunzi wawili wa KPL wameshutumu ghasia hizo na kuwataka mashabiki wa AFC Leopards kuheshimu sheria na kuridhika na matokeo ya mechi.
Naibu Kocha wa Vihiga United Francis Xavier ameonya kwamba vurugu kama hizo zinarejesha nyuma mchezo wa soka nchini na ni tabia ambayo haifai kuvumiliwa tena na Shirikisho la soka FKF.
Naye Boniface Ambani anayekinoa kikosi cha chipukizi wa AFC Leopards amesikitika kwamba hatua ya mashabiki hao itajutiwa sana kutokana na gharama inayoandamana nayo.