Michezo

Yanga matumaini tele italima Rayon na Gor kutinga robo fainali

August 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Geoffrey Anene

YOUNG Africans (Yanga) imeapa kukamilisha kampeni yake ya Kombe la Mashirikisho la Afrika mwaka 2018 kwa kishindo.

Mabingwa hawa mara 27 wa Tanzania wako jijini Kigali nchini Rwanda kukabiliana na wenyeji Rayon Sports katika mechi ya Kundi D.

Katika mahojiano mapema Jumatano, kocha Mwinyi Zahera na nahodha Gadiel Michael wameambia vyombo vya habari nchini Rwanda kwamba Yanga haijasafiri Kigali kutalii tu, bali kupata ushindi.

“Tunalenga kuendelea kushinda. Ndoto yetu ya kuingia robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho la Afrika ilizimwa, lakini ushindi dhidi ya Rayon utatuimarisha kiakili kwa mechi zetu zijazo na pia kuongeza motisha ya kikosi hiki. Lengo letu kubwa ni kushinda Ligi Kuu,” amesema Zahera.

Naye Michael ametangaza, “Motisha kambini iko juu na tuko Kigali kufanya kazi. Kila mchezaji anayepewa fursa ya kuonyesha uwezo wake uwanjani yuko tayari kujitolea kwa dhati kuhakikisha tunakamilisha kampeni vyema.” Yanga ilichapa USM Alger 2-1 Agosti 19 na kucharaza Mtibwa Sugar 2-1 Agosti 23.

Gor Mahia ya Kenya inaongoza kundi hili kwa alama nane sawa na nambari mbili USM Alger kutoka Algeria. Gor na Alger zitalimana jijini Algiers kuanzia saa kumi jioni Jumatano. Rayon ni ya tatu kwa alama sita nayo Yanga imezoa alama nne. Timu mbili za kwanza kutoka kundi hili zitaingia robo-fainali.