Yaya Toure ampigia upatu Didier Drogba awe Rais mpya wa shirikisho la soka Ivory Coast
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO wa zamani wa Barcelona na Manchester City, Yaya Toure anaunga mkono aliyekuwa mfumaji matata wa Chelsea, Didier Drogba kuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast (FIF).
“Huu ndio wakati wa mabadiliko makubwa kufanyika katika soka yetu inayohitaji kuendeshwa kwa mtindo wa kisasa,” akatanguliza Yaya ambaye kwa sasa huchezea kikosi cha Qingdao Huanghai nchini China.
“Ninaposema kwamba namuunga mkono, Drogba, eleweni kwamba ni kwa mustakabali bora wa soka ya Ivory Coast. Pia ni fahari kubwa kuwa na mwanasoka wa hadhi yake akitumikia taifa hili katika kiwango tofauti. Awekeze humu barani Afrika na maarifa yake yafaidi maelfu ya chipukizi wetu,” akaongeza Yaya ambaye ni kakaye beki wa zamani wa Arsenal, Man-City na Liverpool, Kolo Toure, 39.
Drogba ambaye alichezea Ivory Coast katika jumla ya michuano 105 kabla ya kuangika rasmi daluga zake mnamo Agosti 8, 2014, alitangaza nia ya kuwania uenyekiti wa FIF mnamo Septemba 2019.
Ingawa hivyo, uchaguzi mkuu wa FIF umetatizwa na janga la corona ambalo limesitisha shughuli za michezo katika takriban dunia nzima. Hadi kufikia sasa, hakuna tarehe mpya ambayo imetolewa na vinara wa FIF kwa minajili ya uchaguzi huo.
Drogba ambaye hadi kustaafu kwake alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast almaarufu The Elephants, atapimana ubabe na Naibu Rais wa FIF, Idriss Diallo na Sory Diabate ambaye atapania kuhifadhi wadhifa wake katika uongozi wa shirikisho hilo.
Licha ya Yaya kuunga mkono azimio la Drogba, baadhi ya wachezaji wamempinga peupe huku Muungano wa Wanasoka wa Zamani wa Ivory Coast (UFIFP) ukijitokeza kumpigia chapuo Diabate.
Akitumia mtandao wake wa Instagram, Yaya alisema, “Drogba alikuwa nahodha na kakangu mkubwa katika timu ya taifa. Watu walizungumza sana kutuhusu katika kipindi cha usogora wetu kambini mwa kikosi cha Ivory Coast. Hata hivyo, tulisalia kimya, tulidumisha busara na tunafahamiana vyema mno.”
“Watu wengi sana wakiwemo mashabiki na wanahabari walikuwa wepesi wa kumkosoa, kumkejeli na kumbebesha lawama kila mara kikosi kiliposhindwa kutamba katika baadhi ya michuano ya haiba kubwa,” akaongeza Yaya.
Wachezaji wa sasa wa kikosi cha Ivory Coast watakuwa miongoni mwa watakaopiga kura za kuchagua Rais mpya wa FIF.
“Bila shaka atapigiwa kura nyingi kutoka kwa marais wa klabu mbalimbali za soka ya Ivory Coast na Chama cha Wanasoka wa Ivory Coast (AFI). Sidhani kuna yeyote atamkaribia akitia kapuni kura za washikadau hawa wote. Kwa upande wa UFIFP, Drogba ana kura yangu,” akasema.