Zidane sawa na Del Bosque kwa makali – Casillas
NA CECIL ODONGO
MNYAKAJI wa FC Porto Iker Casillas amelinganisha sifa za kocha mpya wa Real Madrid Zinedine Zidane na mkufunzi wa zamani wa timu hiyo Vincente del Bosque, akisema atasaidia Los Blancos kutwaa mataji mengi.
Casillas na Zidane walifundishwa soka na kocha huyo wa zamani wa zidanUhispania aliyesaidia Real Madrid kutwaa UEFA Super Cup, mataji mawili ya La Liga na mengine mawili ya Klabu Bingwa Barani Uropa akiisimamia. Bosque vile vile alishinda kombe la Dunia mwaka 2010 akiwa kocha wa timu ya Taifa ya Uhispania.
Hata hivyo, Casillas ambaye aliwajibikia Real Madrid kwa kipindi cha miaka 16 alisifu kurejea kwa Zidane ambaye alisaidia klabu hiyo kutwaa mataji matatu ya Klabu Bingwa Barani Uropa na ubingwa wa La Liga katika awamu yake ya kwanza ya miaka miwili na nusu kama kocha mkuu.
Ingawa hivyo, alirejea Santiago Bernabeu kuchukua usukani wa ukocha mwezi Machi 2019 baada ya Rais wa klabu Florentina Perez kumtimua Santiago Solari kutokana na misururu ya matokeo duni.
“Ukiwa umewahi kusakata kabumbu na kufikia kiwango cha Zidane basi una ujuzi mkubwa wa jinsi ya kuwashughulikia wachezaji ukiteuliwa kama kocha. Zidane anaifahamu Real Madrid na anaweza kuwadhibiti wachezaji ndiyo maana alifanikiwa sana katika kipindi cha kwanza cha kuhudumu kwake,”
“Huo mtindo wa uongozi wa Zidane ndio ulitumiwa na Vincente del Bosque kati ya mwaka 2000 hadi 2004 alipokuwa mkufunzi wa Real Madrid. Nina imani ataifufua tena timu hiyo na kuiwezesha kutamba kwasababu amerejesha motisha na uwajibikaji uwanjani miongoni mwa wachezaji,” akasema Casillas.
Zidane ameshinda mechi zote tatu alizosimamia tangu marejeo yake, ushindi wa hivi punde ukiwa 3-2 dhidi ya Huesca mnamo Jumapili Machi 31 katika uwanja wao wa nyumbani wa Santiago Bernabeu.