Zion Winners wasema coron haitawazuia kutesa ligini
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Zion Winners ni miongoni vikosi ambavyo hushiriki michuano ambayo huandaliwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Tawi la Nairobi Magharibi. Aidha Zion Winners imeorodheshwa kati ya timu ambazo hushiriki kampeni za Ligi ya Kaunti Nairobi.
Kocha wake, Daniel Vwaya anasema kwamba licha ya wachezaji wake kupoteza makali kutokana na janga la corona ana imani anacho kikosi imara kinachoweza kufanya vizuri kwenye kampeni za kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL).
MSIMU MPYA
”Bila kuwasifia wachezaji wangu wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kampeni za kipute hicho kila muhula lakini huteleza dakika za mwisho na kukosa tiketi ya kusonga mbele,” alisema na kuongeza kuwa licha ya hayo msimu ujao wanalenga kujituma kiume angalau kuibuka kati ya timu mbili za kwanza kwenye jedwali ili kutia kapuni tiketi ya kupanda ngazi.
Mkufunzi huyo anadokeza kuwa kama ilivyo kawaida ya timu zingine tatizo la udhamini ndilo huwatesa pakubwa na kukwamilisha mipango yao michezoni.
Anasema kwa sasa wamenasa chipukizi kadhaa wapya kwenye juhudi za kujiongezea nguvu tayari kwa kipute cha muhula ujao.
UDHAMINI
Naye meneja wake, Isaac Sebhi anasema ”Tumepania kukaza buti kuhakikisha tumefuzu kushiriki soka ya Ligi Kuu Kenya ndani ya miaka sita ijayo.”
Anadokeza kwamba ingawa kikosi hicho kinashiriki soka la viwango vya chini, wachezaji wake wanajiamini wanaweza kufanya vyema ila suala la udhamini limeibuka donda sugu.
Zion Winners ya eneo la Westlands ni kati ya vikosi vingi tu ambavyo viongozi pia wachezaji wavyo hupitia wakati mgumu kuendesha shughuli zao michezoni kwa kukosa mdhamini.
KUZALIWA
”Ninaamini kwamba tungebahatika kupata ufadhili bila shaka tungeonyesha kandanda ya kuvutia dhidi ya wapinzani wetu kinyume na ilivyo sasa,” akasema.
Kadhalika anatoa mwito kwa viongozi wa FKF wazamie zaidi shughuli za kuinua mchezo huo mashinani. Anasema wanastahili kusaka wafadhili kupiga jeki michuano ya vipute vya chini.
Anawashauri kuwa wanapaswa kuelewa timu za mashinani zinahitaji ufadhili zaidi ili kuendesha shughuli zao michezoni. ”Ni ajabu kwamba klabu za mashinani huwa hazihesabiwi katika mgao wa fedha ambazo hutolewa kila mwaka na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA),” akasema.
Timu hiyo iliyoasisiwa mwaka 2008 inajivunia kukuza wachana nyavu wengi tu waliobahatika kuhamia vikosi zingine kwenye juhudi za kusaka matunda mema baada ya kuonyesha soka la kuvutia. Baadhi yao wakiwa: Kennedy Barros (Maua FC Meru) na Daniel Otieno (Sony Sugar).