Dondoo

Mke afinya nyeti za polo wakizozana

October 17th, 2020 1 min read

Na Mwandishi Wetu

KANGEMI, NAIROBI 

JOMBI mmoja mtaani hapa anaendelea kuuguza majeraha kwenye nyeti zake baada ya kushambuliwa na mkewe wakizozania rimoti. Inadaiwa jombi alitoka kazini alasiri na alipofika nyumbani, akapumzika sebuleni tayari kutazama mechi ya ligi ya soka nchini Uingereza.

Wakati huo huo, mkewe aliingia akiwa na shoga yake. Wawili hao walipanga kutazama kipindi cha masuala ya urembo walichokishabikia sana. Mgeni alipompata mume wa rafiki yake, aliondoka moja kwa moja bila kuaga. Duru zinasema mama alimgeukia mumewe.

“Mara ngapi nimekuonya usiiguse rimoti? Tayari mgeni wangu ameondoka! Mbona hivyo jamani?” Mke alilalamika akimpokonya mume rimoti na kuweka stesheni aliyopenda.

Jombi alihisi kudhalilika, akaichukua rimoti tena na kubadilisha chaneli.“Naona umemea pembe eeh! Leo utanitambua,” mke alighadhabika akimzaba kibao kikali.

Wawili hao walikamatana kwa vishindo na kubwagana sakafuni. Kwa kuwa mke alikuwa kibonge, ilikuwa rahisi kumlemea mumewe.

Inadaiwa jombi alikabwa koo alipojaribu kupiga nduru na kufinywa nyeti. “Mama, tafadhali usimuumize dadi. Msamehe tu hatarudia tena,” mtoto alimsihi mama yake alipoingia sebuleni na kushuhudia yaliyokuwa yakiendelea.

“Toka nje mara moja,” mama aliamuru naye mtoto akatii. Alipotoka, aliwaita majirani kadhaa ambao waliingia katika nyumba kumwokoa kalameni.Walimpata jombi akiomba msamaha na kumlilia mkewe amwachilie.

“Si vyema kupigana kwa ajili ya rimoti. Nyinyi ni watu wazima. Si vyema pia kupigana mbele ya mtoto wenu,” jirani mmoja alisema akiinama kumwuokoa jombi.

Duru zinasema majirani walikuwa na wakati mgumu kumnyanyua mke wa jombi mwenye uzito wa nanga ambaye alikataa kumwachilia mumewe, akidai alitaka kumtia adabu. Jombi alipoachiliwa alishindwa kusimama, akilia huku mikono ikiwa kwenye nyeti zake

.“Sitamwonea huruma na wallahi kama msingefika, ningemng’oa ‘mlingoti’. Hapa ni kwangu,” mke alisema tamko ambalo liliwashangaza majirani.