Makala

Sababu kuu naunga maandamano ni kwamba mke wangu ni Gen Z – Pasta Ng’ang’a

Na FRIDAH OKACHI July 18th, 2024 1 min read

MHUBIRI wa kanisa la Neno Evangelism, Bw James Ng’ang’a kwa mara nyingine ametetea msimamo wake wa kuunga mkono maandamano ya vijana almaarufu Gen Z yanayolenga kuiwajibisha serikali.

Wakati wa mahojiano, mchungaji huyo alifichua alipata msukumo kutoka kwa mkewe Gen Z, ambaye hufanya maandamano na vijana wengine kupinga uongozi mbaya na ufisadi kutoka kwa maafisa wa serikali.

“Bibi yangu alikufa na nikaonekaniwa na kuoa Gen Z, huwa anaenda kwenye maandamano na kugongwa na vitoa machozi,” alifichua Pasta Ng’ang’a.

Pasta Ng’ang’a alitaja msimamo wa kuunga mkono kizazi cha Gen Z unatokana na ukakamavu wa kuzungumzia wazee ambao usemi wao haungesikilizwa.

Mchungaji huyo alisema kutozungumza kwake dhidi ya serikali kwa njia yoyote ile ni kwa sababu vijana wanamzungumzia.

“Mimi niko pamoja na Gen Z, niko hapo. Walisema eti nisiende kwenye maandamano yao eti nitapigwa na vitoa machozi nife. Lakini enyewe safari hii mmetupasha tohara kwa mara ya pili. Hatuongei sisi wazee, tuko na dawa za kupunguza maumivu (Panadol) kwa mfuko,” alisema Bw Ng’ang’a.

Kwa utani, Ng’ang’a alipelekwa mahakamani kwa tuhuma za kuzungumzia vibaya serikali. Kulingana naye atakapofika kizimbani, atasingizia umri wake na kumuambia hakimu kwamba huenda alizungumza wakati shinikizo la damu lilikuwa limeongezeka.

“Mimi sijaongea mambo ya serikali, usiniletee wazimu wako. Mimi niko na umri wa miaka 71, hata ukinipeleka mahakamani nitaambia hakimu presha ilikuwa juu. Presha ya wazee huwa wakati mwingine ni yale maneno mtu huzungumza bila kujua,” aliongeza huku akicheka.

Baada ya Rais Ruto kutimua mawaziri wake, mchungaji huyo alionekana kwenye video akimkejeli aliyekuwa waziri wa Usalama wa ndani Bw Kithure Kindiki.