Michezo

‘Mlimnunua Jadon Sancho mkashindwa kumtumia’

May 2nd, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

KLABU ya Borussia Dortmund inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani imerusha cheche kwa klabu mojawapo, ikidai inafaa kumuomba msamaha Mwingereza Jadon Sancho.

Dortmund baada ya kutandika Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (Uefa), mnamo Jumatano, walichapisha kwenye ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) kuwa Sancho angali katika ubora wake.

“Nyinyi nyote mnafaa kumwomba (Jadon Sancho) msamaha. Tumekuwa tukielewa mchezo wake wakati wote,” chapisho la klabu hiyo likasema.

Ingawa walioelekezewa ujumbe huo hawakutajwa, ni vyema ifahamike Sancho aliondoka uwanjani Signal Iduna Park kuenda nchini Uingereza kuwajibikia klabu ya Manchester United. Akiwa pale Old Trafford, fomu yake ilionekana kuwa chini, hali iliyomlazimu kurejea kwa waajiri wake wa zamani.

Akiwa pale Man U, alikosana na kocha Erik ten Hag na kuishia kupigwa marufuku asichezee klabu hiyo inayofahamika kiutani kama The Red Devils hadi aombe msamaha.

Kitumbua kilipoingia mchanga, Sancho alilazimika kushiriki mazoezi na machipukizi wa Man U.

Kabla ya kuhamishwa, Sancho alimkaripia Ten Hag hadharani baada ya kocha huyo kumkosoa alipozungumza na vyombo vya habari.

Kocha huyo alisisitiza hakuridhishwa na mchezo wake Sancho lakini baada ya kuhamishwa kwenda Ujerumani, mwanasoka huyo wa Uingereza amekuwa akifana na sasa anashiriki Uefa katika mkondo wa nusu fainali.

Ten Hag aliwahi kuulizwa na wanahabari kuhusu fomu ya Sancho akiwa Bundesliga (Ligi ya Ujerumani) ila alipuuza hilo halikuwa suala kuhusu mzozo wao.

“Lakini tunajua Jadon Sancho ni mchezaji mzuri sana na kwa hivyo hilo halitushangazi. Suala si hilo,” alisema Ten Hag.