Michezo

Mnyama Haaland ‘aua Arsenal’ kwa kuongoza Man City kukomoa Wolves 5-1

May 4th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BAADA ya mashabiki wa Arsenal kutegemea Wolverhampton Wonderers (Wolves) iwashikie Manchester City katika mchuano wa kuwania taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Etihad pasipo ufanisi wowote, sasa wamesema ni sawa tu, Mungu mbele.

Kwa kiwango kikuu, wafuasi wa Arsenal wanamwona mchezaji Erling Haaland kuwa mnyama katili wa soka ugani baada ya kutikisa nyavu mara nne na kuongoza Man City kuikomoa Wolves kwa magoli 5-1, la tano likifungwa na Julian Alvarez katika dakika ya 85.

Bao la Wolves la kufutia machozi lilitiwa kimiani na mchezaji Hwang Hee-Chan katika dakika ya 53.

Matokeo hayo yaliinua Man City hadi pointi moja nyuma ya Arsenal (83/82) katika jedwali.

Man City walikuwa nyumbani, hali ambayo iliyafanya maombi ya Arsenal kwamba Wolves ifanye mambo kuwa sawa na kumkama kuku upate maziwa ya kupikia chai au ya kugadisha upate mala.

Matokeo hayo yanazidisha presha kwa Arsenal ambayo inasaka taji hilo la EPL ambalo limewahepa kwa miaka 20 sasa, huku Man City ikilisaka kwa mara ya sita mfululizo.

Huku Man City kwa sasa ikibakia na nafasi ya kuzoa alama tisa katika mechi tatu iliyosalia nazo, Arsenal imebakia kusaka pointi sita. Huku Man City kwa sasa ikiwa na pointi 82, ina maana kwamba ikifanikiwa kuzoa zilizobaki tisa, itajipa ubingwa kwa pointi 91.

Arsenal kwa sasa ikiwa na pointi 83 ina uwezo tu wa kujipa pointi 89 iwapo itashida zote mbili zilizosalia.

Mashabiki wa Arsenal wanatarajia kwa kila aina ya maombi kwamba Man City iangushwe angalau mara moja ndipo usakaji wa ubingwa huo wa EPL uwe katika mazingara yaliyo na usawa.

Kwa sasa, mechi za Man City ambazo zimesalia ni dhidi ya Fulham, Tottenham Hotspur na West Ham United huku Arsenal ikibakisha kumaliza udhia na watani wao wakuu Manchester United na kisha Everton.

Lakini Man City imeonekana kuwa na makali ya ukatili katika kukimbizana na taji hilo awamu hii ya lala salama, hivyo basi kuwafanya Wanabunduki Arsenal almaarufu The Gunners, kuonelea kana kwamba kani ya kuwapa taji imesombwa na mafuriko yanayoendelea katika maeneo mengi nchini Kenya na duniani kwa ujumla.