Habari za Kitaifa

Mshtuko, uchungu wazazi wakipoteza watoto kwenye mkasa wa moto shuleni


MSHTUKO, uchungu, huzuni, maswali kuhusu ‘ni nini kilitokea’ yalisumbua wazazi wa wanafunzi wa shule ya Hillside Endarasha Academy, katika Kaunti ya Nyeri, ambapo wanafunzi 17 walifariki na 13 kujeruhiwa katika mkasa wa moto katika bweni la wavulana.

Moto huo uliozuka katika bweni moja la wavulana 156 katika shule hiyo ya mseto, ulianza mwendo wa saa tano usiku.

Waliokuwa wa kwanza kufika shuleni walieleza taswira ya kutisha ambapo wanafunzi walikuwa wamenaswa ndani ya bweni huku wale waliofanikiwa kutoka nje wakiruka ukuta kutoroka moto huo.

John Mugo, ambaye alifika shuleni mwendo wa saa sita usiku alisema alikuwa ameenda kufuatilia mtoto wa dadake wa darasa la saba.

“Tulijaribu tuwezavyo kuokoa watoto. Baadhi ya wakazi walihatarisha maisha na kuloweshwa blanketi kwenye maji, wakajifunika na kuingia ndani ya bweni. Niliona kadhaa wakitoka kwenye moto huo kila mmoja akiwa ameshika mtoto. Lilikuwa tukio baya,” Bw Mugo alisema na kuongeza kuwa moto huo ulichochewa na upepo mkali.

Wakati wa mahojiano, Bw Mugo alikuwa bado na matumaini kuwa mpwa wake alikuwa hai.

“Tunashikilia matumaini kuwa mtoto wetu yuko hai,” alisema.

Hata hivyo, alionyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya bweni akisema wanafunzi walikuwa wamejaa.

“Dada yangu alipomleta mwanawe aliniambia kuwa alikuwa na wasiwasi kuhusu bweni, alisema walikuwa wamesongamana,” aliongeza.

Philip Gathogo ambaye alifika shuleni mwendo wa saa 12:30 asubuhi alisema sehemu moja ya kuta za bweni ilijengwa kwa mbao.

“Moto huo ulianzia kwenye sehemu hiyo uliwaka kwa kiwango ambacho hatukuweza kuuzima. Baadaye, wazima moto walifika na tukafanikiwa kuuzima,” alisema.

Alisema katika juhudi kubwa za kuwaokoa watoto hao, pia walibomoa sehemu za kuta.

Wazazi wengine waliosafiri kutoka Nairobi walisema walifahamu kisa hicho alfajiri.

“Nilipigiwa simu usiku sana lakini sikupokea kwani nilikuwa nimelala. Namshukuru Mungu mwanangu yuko salama,” alisema Mary Mbula.

Bw Derrick Kiama, mzazi ambaye mtoto wake wa kiume wa darasa la sita alibahatika kuwa hai, anasema kuwa alipata habari kuhusu moto huo kutoka kwa mzazi mwenzake Alhamisi usiku, Septemba 5, 2024.

Alisema mzazi huyo alimpigia simu majira ya saa sita usiku akisema amemchukua mtoto wake kutoka shuleni na yuko salama kwake.

“Nilimwambia amchukue mwanangu nyumbani na kukaa naye hadi asubuhi,” alisema, akiongeza kuwa aliamua kukaa shuleni kusaidia familia za watoto walioathirika.

Bw John Rukwaru ambaye hakuwa amejua hatima ya mjukuu wake kufikia wakati wa kwenda mitamboni alisema alipigiwa simu saa tano usiku na kuambiwa kuwa bweni lilikuwa likiteketea.

“Tulijaribu kuzima moto lakini ulikuwa mwingi. Kufikia wakati magari ya zima moto yanapowasili moto ulikuwa umeteketeza bweni,” alisema.

Wakati fulani, wazazi waliokuwa na wasiwasi walitishia kuingia lilipokuwa bweni lililotengwa kama la uhalifu wakisema walikuwa wamefungiwa katika mojawapo ya madarasa kwa muda mrefu bila habari zozote.

Kamishna wa Kaunti ya Nyeri ambaye pia ni kaimu kamishna wa eneo hilo Bw Pius Murugu alisema kuwa timu ya wachunguzi kwa sasa inasubiri mtaalamu wa maiti wa serikali kutathmini eneo la tukio.

Alisema changamoto kubwa ambayo timu hiyo ilikabiliana nayo tangu Ijumaa asubuhi, Septemba 6, 2024 ni kujaribu kuhesabu watoto wote 156 waliokuwa bwenini.

“Tuna habari kuwa kuna watoto waliofanikiwa kuruka ua wa shule huku wengine wakinaswa ndani ya bweni la shule. Timu ya DCI iko hapa kujua ni nini hasa kilifanyika,” alisema.

Haya yanajiri huku baadhi ya wazazi wakilalamika kwamba hawakuwa na taarifa kuhusu wanafunzi waliolazwa hospitalini.

Katibu wa Elimu Belio Kipsang, ambaye alizuru eneo la tukio, alisema eneo hilo lilikuwa la kutisha.

“Nimepata fursa ya kutembelea eneo la tukio. Inasikitisha sana kwamba watoto wetu walipitia aina hiyo ya maumivu. Serikali imetuma mashirika yote ya usalama ikiwa ni pamoja na maafisa wa DCI ambao watachunguza na kubaini chanzo cha moto huo,” akasema.