Habari za Kaunti

Mtoto wa miaka 4 kati ya waliopigwa risasi katika maandamano Karatina

Na STEPHEN MUNYIRI August 12th, 2024 2 min read

KATIKA maandamano ya hivi karibuni mjini Karatina Kaunti ya Nyeri, msichana mwenye umri wa miaka minne alikuwa kati ya zaidi ya watu 20 waliopigwa risasi na kujeruhiwa.

Polisi nao wanasema kuwa wenzao watano walijeruhiwa na magari yao mawili kuharibiwa vioo.  Wale ambao wamelazwa katika Hospitali ya Karatina baada ya kupigwa risasi na polisi ni Ivana Gathigia (miaka minne) Eric Waigwa (23), Brian Mwangi(28), Sarah Githinji(52), Baxton Mwangi (35), Kelvin Gicheru (19) na   Cynthia Mera (19).

Mwengine ambaye alijeruhiwa ni Wycliffe Thiong’o (25) ambaye ni msusi mjini humo na amehamishwa hadi Hospitali ya Kenyatta kwa matibabu zaidi.

Taifa Leo ilipozuru hospitali hiyo mnamo Jumamosi, baadhi ya waathiriwa bado walikuwa na risasi katika miili yao wakisubiri kufanyiwa upasuaji.

Ivana, 4, alikuwa na bandeji katika mkono wake wa kulia na uchunguzi wa miale ya X ray ulionyesha kuwa bado kulikuwa na kifaa kilichokuwa ndani ya mkono wake.

Mamake Eunice Githiga alimtoa mwanawe kutoka kituo kimoja cha malezi ambako yeye humwacha kisha wakaanza kutembea kwenda nyumbani.

Baada ya muda, polisi walianza kufyatua risasi kiholela na katika harakati za kujiokoa, mwanawe alimponyoka na hapo ndipo akapigwa risasi.

Risasi hiyo haikumpata moja kwa moja kwani ilipiga ukuta kwanza kisha ikamgonga.

Bi Githiga alisimulia kuwa alizimia baada ya risasi hiyo kumgonga mwanawe kwa kuwa alifikiria  alikuwa ameaga dunia.

Alipopata fahamu baadaye rafiki yake alimweleza kuwa Ivana alikuwa amekimbizwa hospitalini ambako alikuwa amelazwa.

“Ni kwa neema ya Mungu kuwa bado yupo hai kwa kuwa hali ingekuwa mbaya zaidi kama risasi ingempata. Sidhani kuwa polisi walikuwa wakimlenga ila kilichotokea kwake hakifai na kimeniogofya sana pamoja na msichana wangu,” akasema.

Waathiriwa wengine walisimulia jinsi walivyopatikana na risasi hizo huku wakikanusha kuwa walikuwa wakishiriki maandamano.

Waathiriwa wawili wapo kwenye hali hatari kutokana na majeraha tumboni na kifuani.

Vile vile, wengine walipata majeraha miguuni baada ya polisi kuwapiga risasi wakati wa maandamano hayo.

Mkurugenzi wa Matibabu katika Kaunti ya Nyeri Dkt Nelson Muriu alisema kuwa idara ya afya ilikuwa imewatuma wahudumu kuwashughulikia wenye majeraha ya risasi.

Kamanda wa Polisi wa Mathira Mashariki Samson Leweri ambaye pia alijeruhiwa akikabiliana na waandamanaji alisema wenzake watano pia walipata majeraha baada ya kupigwa mawe.

Kupigwa kwa waandamanaji risasi kunatokea wiki moja baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kuamrisha vyombo vya usalama vikomeshe maandamano hayo yanayotokea katika ngome yake ya kisiasa.

 Kati ya 2017-2022, Bw Gachagua alihudumu kama mbunge wa Mathira ambako mji wa Karatina unapatikana.