Habari

Mtunza bustani nyumbani kwa Moi asema kiongozi huyo alipenda kusuluhisha mambo upesi

February 7th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

ALIPOKUWA Rais, Daniel Toroitich Arap Moi alikuwa kiongozi mkakamavu machoni pa umma huku nyumbani akipenda kuyashughulikia mambo upesi.

Bw Hassan Paul ambaye alifanya kazi katika bustani ya maua na kupanda miti nyumbani kwake Rais Moi wiki hii alisimulia kuwa mwajiri wake alipenda kusuluhisha mambo bila kupoteza muda.

Bw Paul alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 40 hadi mwaka 2019 ambapo aliamua kustaafu.

“Kila ulipomkosea Moi, alikuwa anakuita chumbani kwake ambapo alikukaripia na kukukemea na kisha kusuluhisha jambo hilo. Ukiondoka chumbani himo mlikuwa tayari mmeweka sawa mambo,” alisema Bw Paul.

Alisimulia jinsi Moi alivyoamuru ajengewe nyumba ya mbao ambapo aliwekewa simu ambayo Moi alikuwa akimpigia moja kwa moja kumjulia hali na kila alipokuwa akitaka kumwambia jambo.

Bw Paul anasema kuwa atamkumbuka kwa ukarimu wake.

Kazi yake kama mtunza bustani ilimfanya kumjua Rais Moi kwa undani hasa ukarimu wake aliowaonyesha waliokuwa wakikaa karibu naye.

“Alihakikisha kuwa kila siku ya Alhamisi ninaletewa mikate ambayo ingenisukuma wiki nzima,” alisema Paul.

Hata hivyo, Bw Paul anasema kuwa Moi alikuwa hawezi kumwamini mtu kwa urahisi na aliowaamini, aliwatunza kwa karibu.

“Aliamini kuwa idadi kubwa ya watu wenye elimu ya juu waliitumia vibaya hata kufanya utapeli na hivyo, idadi kubwa ya wafanyakazi wake aghalabu hawakuwa na viwango vya juu vya elimu,” akasema Bw Paul.