Habari

Mwaita azimwa kudai shamba la Karen la Sh50 milioni

Na RICHARD MUNGUTI August 24th, 2024 2 min read

ALIYEKUWA Mbunge wa Baringo ya Kati Sammy Mwaita amezimwa na Mahakama Kuu kuingilia umiliki wa shamba la thamani ya Sh50milioni ambalo mfanyabiashara ameshtakiwa kula njama ya kuinyakua.

Mwaita na Howard Mururu Mugambi wanang’ang’ania umiliki wa shamba hilo

Jaji (mstaafu) Joseph Mbalu Mutava anayemwakilisha Mugambi alipinga hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kumshtaki mwekezaji huyo kwa uhalifu akisema “hatua hiyo inakinzana na sheria.”

Bw Mutava alipinga hatua ya DPP kumfungulia mashtaka ya uhalifu Bw Mugambi aliyesema ndiye mmiliki wa shamba hilo lililoko mtaa wa kifahari wa Karen Kaunti ya Nairobi.

Bw Mutava alimweleza hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Susan Shitubi kwamba upande wa mashtaka unatumia vibaya mamlaka ya mahakama kwa kumfungulia mashtaka Bw Mugambi.

“Naomba hii mahakama isitishe kesi ya uhalifu aliyoshtakiwa Bw Mugambi kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu inayosikiza kesi itakayoamua mmiliki halisi wa shamba hilo la Karen. Kesi inasikizwa na Jaji Jacquline Mogeni,” Bi Shitubi alifahamishwa na Bw Mutava.

Mahakama iliendelea kufahamishwa kwamba katika kesi iliyoko Mahakama kuu, Bw Mwaita na kampuni ya Mart Properties Limited wameshtakiwa na Bw Mugambi.

“Mahakama kuu imemzima Bw Mwaita kudai na kuvuruga umiliki wa shamba hilo Nambari 13791/3 lake Bw Mugambi hadi Mahakama kuu itakapoamua mmiliki halisi wa shamba hilo,” Bw Mutava alimweleza hakimu.

Hakimu alifahamishwa na Bw Mutava kwamba Bw Mugambi alinunua shamba hilo kutoka kwa kampuni ya Mart Property Limited mnamo Novemba 18,2021.

“Shamba hili ni lake mshtakiwa huyu (Mugambi)  kwa vile aliinunua  kutoka kwa kampuni ya Mart Property Limited kwa bei ya Sh50milioni,” Bw Mutava alieleza korti.

“Naomba hii mahakama ifutilie mbali kesi hii aliyoshtakiwa Bw Mugambi na DPP. Muda mahususi wa mahakama haupasi kupotezwa kusikiza kesi hii ya umiliki wa shamba ambalo mahakama imemtambua mshtakiwa kuwa mmiliki,” Bw Mutava alisema.

Wakili huyo alisema:“Muda wa mahakama wapasa kutumika tu katika kufanikisha haki na wala sio kuharibiwa kwa kuzinduliwa kwa kesi inayosikizwa na Mahakama Kuu,” Bw Mutava alieleza hakimu mkuu.

Bi Shitubi alimwachilia Bw Mugambi kwa dhamana ya Sh100,000 na kutenga Septemba 4,2024 siku ya kuamua ikiwa mshtakiwa atasomewa shtaka hilo au la.

[email protected].