Habari za Kitaifa

Mzozo wa Safaricom na Starlink ya Elon Musk watua kortini


MZOZO wa kibiashara kati ya kampuni ya mawasiliano ya Safaricom na Starlink  ya bilionea wa Amerika Elon Musk umefika kortini.

Shirika la Kituo cha Sheria linataka Starlink iruhusiwe kuhudumu nchini tofauti na Safaricom inayozua wasiwasi kuhusu kampuni hiyo ya kutoa huduma za mtandao.

Katika kesi ya dharura, shirika hilo lisilo la kiserikali linasema huduma za intaneti zinapaswa kuruhisiwa kukua  na madai ya Safaricom  kwamba kuingia moja kwa moja kwa Starlink katika Kenya ni tishio kwa usalama wa mtandao hayana msingi.

Kituo Cha Sheria kinasema katika kesi yake kwamba madai ya Safaricom katika barua iliyoandikwa Julai 5 2024 kwa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) hayakufafanuliwa.

Kupitia wakili Marc Chirchir, shirika hilo linataka mahakama iagize Mamlaka ya Ushindani wa Kibiashara  ya Kenya (CAK) na CA  na mashirika mengine ya udhibiti  kufanya uchunguzi wa kisayansi na utafiti, usioshawishiwa kwa vyovyote kuhusu mbinu bora zaidi za huduma za intaneti kupitia setilaiti kabla ya kuimarisha sheria kuzihusu.

“Kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, agizo litolewe kuzuia mshtakiwa wa pili na wa tatu (CA na CAK)  kuchukua hatua zozote ambazo zinaweza kuathiri wanaotumia Starlink ya  SpaceX ikiwemo  kuzima malipo yoyote kwa Starlink, kampuni washirika wake na wasambazaji,” anasema Bw Chirchir.

Safaricom inataka CA kuchunguza uamuzi wa kutoa leseni kwa kampuni huru za kutoa huduma za intaneti kupitia setilaiti ikionya kuwa inaweza kuruhusu uunganishaji haramu na kuvuruga mawasiliano ya simu.