• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Chania High yapokea Sh10 milioni kutoka kwa Rais

Chania High yapokea Sh10 milioni kutoka kwa Rais

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE ya upili ya Chania High ya Thika imepokea Sh10 milioni kutoka kwa Rais William Ruto alizotoa zitumike kama za mchango wa kujenga mabweni ya wanafunzi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw James Gitau aliitisha Harambee ambapo mgeni wa heshima alikuwa Katibu wa Wizara ya Elimu Dkt Belio Kipsang’.

Bw Gitau alisema licha ya shule kupitia changamoto ya ukosefu wa mabweni, bado shule hiyo inafanya vizuri katika matokeo ya mitihani wa kitaifa, ambapo watahiniwa wa KCSE 2022 walitia fora.

“Licha ya wanafunzi hawa kulala chini ya mahema, bado walionyesha ni moto wa kuotea mbali,” alisema mwalimu mkuu Bw Gitau.

Alisema walihitaji takribani Sh40 milioni ili kukamilisha ujenzi wa mabweni yote ya wanafunzi shuleni humo.

Kampuni kadhaa, zikiwemo Broadway, Capwell, miongoni mwa nyingine, zilichanga zaidi ya Sh7 milioni.

Hazina ya maendeleo ya NG-CDF kupitia mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a ilitoa Sh4.6 milioni.

Wengine waliotoa michango yao ni wazazi, wageni waheshiwa na wanafunzi wa zamani wa Chania High waliotoa Sh2 milioni.

Dkt Kipsang’ alisema masomo ya Sayansi na Teknolojia yana umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa sasa.

“Tunataka katika siku zijazo wanafunzi wawe na ujuzi wa maswala ya Sayansi na Teknolojia,” alisema Dkt Kipsang’.

Alisema vyuo vya kozi anuwai almaarufu TVET vina umuhimu wa kuwahami wanafunzi na ujuzi wanaohitaji ili kupata ajira.

Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyiro, ambaye ni mwenyekiti Kamati ya Bajeti Bungeni, alisema serikali ilitenga takribani Sh630 bilioni za maswala ya elimu katika bajeti iliyosonwa majuzi ya mwaka wa kifedha wa 2023/24.

Alisema serikali ina mipango kabambe  katika sekta ya elimu na kwa hivyo wazazi wasiwe na wasiwasi wowote.

“Mimi ninawahimiza nyinyi wanafunzi mfanye bidii katika masomo ili maisha ya baadaye yawe mazuri kwenu.” alisema Bw Nyoro.

Naye Bi Ng’ang’a alisema masomo ni muhimu kwa kila mwanafunzi kwa sababu yanasawazisha na kufanya kila mwanafunzi awe na fursa sawa na mwingine, mradi tu amakinike na kutumia fursa zilizoko.

“Jukumu kubwa la mzazi kwa mwanafunzi ni kumpatia elimu kwa maisha yake ya baadaye,” alisema mbunge huyo.

Alisema ataendelea kushirikiana na shule ya Chania kwa maswala yote yenye umuhimu mkubwa kwa jamii.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens watinga nusu fainali Dimba la CECAFA

Urithi: Mjane atabasamu serikali ikimsaidia kunasua...

T L