Habari za Kitaifa

Ngoja ngoja yaumiza matumbo Ruto akiteua kamati kutathmini mfumo tata wa ufadhili vyuoni

Na DAVID MUCHUNGUH September 16th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto ameteua kamati ya watu 129 kushughulikia mfumo wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu ambao umeshutumiwa vikali ukidaiwa kuongeza gharama ya elimu na kuwatenga wanafunzi kutoka familia maskini.

Katika notisi maalum iliyochapishwa, Rais ametangaza kubuniwa kwa Kamati ya Kitaifa kuhusu Tathmini ya Mpango Mpya wa Kufadhili Elimu ya Chuo Kikuu.

Kamati hiyo inayojumuisha wanachama kutoka sekta tofauti tofauti ikiwemo wanafunzi wa chuo kikuu itaongozwa na aliyekuwa katibu wa wizara, Profesa Japheth Micheni Ntiba.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu Julius Ogamba aliwasihi wanafunzi wa chuo kikuu kusitisha mgomo wa kitaifa uliopangwa kuanza Septemba 9 2024, kupinga mfumo huo.

Aliahidi wanafunzi kuwa kamati itaundwa kutathmini mfumo huo ulioanzishwa mwaka uliopita.

Tangazo hilo limejiri vilevile siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mgomo wa kitaifa uliotangazwa na wahadhiri wa vyuo vikuu kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Mishahara (CBA) 2021 – 2025.

Maafisa wa kitaifa wa Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (Uasu) walishiriki mazungumzo na Bw Ogamba Jumatatu lakini matokeo yake hayakuwa yametolewa habari hizi zilipokuwa zikichapishwa.

Kulingana na notisi rasmi, kamati hiyo itajumuisha vitengo vinne vyenye uongozi na wanachama wake binafsi kila kimoja.

Vitengo hivi vinajumuisha Kundi linaloshughulikia Tathmini na Kupiga Msasa Mpango Mpya kuhusu Elimu na Mafunzo ya Vyuo Vikuu, Vyuo vya Kiufundi na vituo vya Mafunzo, litakaloongozwa na Profesa Karuti Kanyinga, akishirikiana na naibu mwenyekiti Dibora Zainab.

Kundi linaloshughulikia Rufaa zinazoibuka kutokana na uainishaji wa wanafunzi katika makundi mbalimbali ya kutengewa ufadhili na mikopo ambalo mwenyekiti wake ni Walubengo Waningilo, na mwenyekiti mwenza, Lucy Machugu.

Dkt Ruto alimteua Robert Oduor Otieno kuwa mwenyekiti wa Kundi linalosimamia Mikopo ya Wanafunzi na naibu mwenyekiti Aaron Kiprotich Bett huku Profesa Mohamed S. Rajab akiwa mwenyekiti wa Kitengo cha Kutathmini Gharama ya Kozi za Masomo ya Vyuo Vikuu akishirikiana na Patrick Malanga.

Wenyekiti na manaibu wenyekiti wa vitengo vya kazi pamoja na Profesa Ntiba watajumuisha bodi ya kamati inayosimamia mipangilio.