Makala

Northern Bypass: Barabara inayozidi kumeza wapitanjia 

January 15th, 2024 1 min read

NA SAMMY WAWERU

NORTHERN Bypass, ni barabara yenye shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi. 

Barabara hiyo ndiyo inaunganisha mtaa wa Ruiru, Kahawa West, na Ngumba, kuelekea hadi Kiambu Road na Ruaka.

Hata hivyo, barabara hiyo katika makutano ya Kamiti Road imegeuka kuwa zimwi la mauaji wenyeji wakilalamikia kupoteza wapendwa wao.

Pasta Harisson Kibira, ambaye ni Kasisi wa Kanisa la AIPCA, tawi la Githurai, anasema kuanzia 2018 barabara hiyo hatari imeangamiza zaidi ya watu 70.

Eneo hatari zaidi ni Jordan-Budalangi, ambalo lina majengo ya kuishi pande zote mbili – Githurai 44 na Kahawa West.

Magari yakipita kwa kasi katika barabara ya Northern Bypass. PICHA|SAMMY WAWERU

“Hapa tumepoteza makumi ya watu wanapovuka barabara kwa kugongwa na magari,” Mchungaji Kibira akaambia Taifa Leo Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Unaposimama dakika kadhaa kujiangalilia, magari yanaonekana yakipita kwa kasi, matrela yakizua hofu zaidi.

Aidha, magari hayaonekana kujali usalama wa wanaovuka barabara.

Eneo hilo la mkasa halina matuta, ‘daraja’ lililopo likiwa mpito wa Kamiti Road kutoka Kahawa West kueleka mtaa wa Githurai 44, Zimmerman na Roysambu.

“Majira ya usiku, wanaovuka bila uangalifu hugigwa dafrau na magari yanayopita kwa kasi,” Nancy Wanja anasema, akisikitika kushuhudia visa kadhaa.

Barabara ya Northern Bypass haina matuta. PICHA|SAMMY WAWERRU

Walevi, Wanja anasema visa vyao vinaongeza kwa wanaogongwa na kufariki wahusika – madereva wakitoroka.

Wanafunzi pia wameathirika pakubwa, Kasisi Kibira akikadiria kiwango kisichojulikana cha watoto kuangamia.

Kando ya barabara hiyo hatari ni shule ya msingi ya kibinafsi ya Green Angels Junior.

Mhubiri Kibira anasema jitihada kuwasilisha malalamishi ya wenyeji kwa Halmashauri ya Barabara za Mijini (KURA), zimegonga mwamba.

Shule ya msingi ya kibinafsi ya Green Angels Junior iliyoko kandokando mwa barabara hatari ya Northern Bypass. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tumejaribu juu chini kushinikiza serikali ituwekee matuta au daraja la watu kuvukia ila malalamiko yetu hayajawahi kuskika,” akasema.

Mwaka 2020, wahubiri wa madhehebu mbalimbali eneo hilo walifanya maombi ya pamoja kutakasa barabara hiyo ili kuondoa mikosi ya ajali za mara kwa mara.

Cha kusitikitisha zaidi, ni kwamba Northern Bypass eneo linalotajwa kuwa hatari halina alama (kibango) cha barabara kutahadharisha madereva kuhusu wapita njia.

Matatu ikisubiri abiria katika eneo hatari la Northern Bypass. PICHA|SAMMY WAWERU