Michezo

Omanyala hajakata tamaa licha ya kushindwa 100m Olimpiki


MTIMKAJI wa mbio za masafa mafupi, Ferdinand Omanyala hajakata tamaa huku akiamini kurejea kwa kishindo na kushangaza Walimwengu hivi karibuni.

Akizungumza baada ya kumaliza katika nafasi ya nane Jumapili kwenye nusu-fainali katika Michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Ufaransa, Omanyala alisema licha ya kukosa kusonga mbele katika mbio hizo fupi, hajakata tamaa kuwania ubingwa katika mashindano mengine yoyote makubwa.

Bingwa huyo wa Afrika alitarajiwa kupata matokeo mazuri, baada ya hapo awali kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mchujo wake uliojumuisha mabingwa kadhaa wanaoshikilia mataji mbalimbali ya kimataifa.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28, alimaliza mbio za Jumapili katika muda wa sekunde 10.08, muda ambao aliutumia kushinda mbio za mchujo wa kufuzu.

Alitumia muda wa 9.79 na kuweka rekodi ya kuwa mkimbiaji wa pili wa muda wa kasi zaidi, nyuma ya Kishane Thompson (9.77).

Baadaye, taji la Paris 2024 lilinyakuliwa na Noah Lyles wa Amerika aliyemaliza kwa muda wa 9.79, akifuatwa na Thompson wa Jamaica aliyekuwa na muda wa 9.79 na Fred Kerley (Amerika, 9.81).