• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Manchester United hoi Arsenal ikifinya Barca kirafiki

Manchester United hoi Arsenal ikifinya Barca kirafiki

NA MASHIRIKA

KIPA wa zamani wa Manchester United, Ben Foster anaamini Erik ten Hag angeendelea kumdumisha David de Gea badala ya kujaza nafasi yake na Andre Onana.

Mashetani hao wekundu walilimwa 2-0 na Real Madrid ugani NRG jimboni Texas, Amerika katika mechi ya kwanza ya Onana hapo jana, kupitia mabao ya Jude Bellingham na Joselu.

Bellingham, ambaye ni mwanasoka ghali kutoka Uingereza baada ya kujiunga na Madrid kutoka Borussia Dortmund kwa Sh21.1 bilioni mwezi Juni, alimbwaga Onana dakika ya tano.

Arsenal walipepeta Barcelona 5-3 katika mechi nyingine kubwa ya kirafiki kupitia mabao ya Bukayo Saka, ambaye pia alipoteza penalti, Kai Havertz, Fabio Vieira na Leandro Trossard (mawili).

Robert Lewandowski, Raphinha na Ferran Torres ndio walifungia Barca uwanjani SoFi jimboni Los Angeles. Onana alipangua makombora kadhaa makali kutoka kwa Madrid kabla ya kufungwa tena dakika za lala-salama kupitia kwa Joselu mbele ya mashabiki 67, 801.

De Gea,32, kwa sasa hana klabu baada ya kandarasi yake kukatika Juni 30 na kocha Ten Hag aliamua kwamba anataka kipa anayecheza kutoka nyuma, ndipo akisaini Onana kutoka Inter Milan kwa Sh8.6 bilioni.

Mholanzi Ten Hag alisema kuwa uwezo wa Onana, 27, akiwa na mpira miguuni pake utabadilisha inavyocheza timu yake.

Hata hivyo, Foster anaamini kuwa fedha ambazo United ilimwaga sokoni kumpata Onana zingetumiwa vyema kwingineko. Na ingawa anakiri kuwa ni hatua nzuri kukimbilia huduma za kipa wa kisasa kama Onana, Foster anahofia kuhusu iwapo wachezaji wengine wa United wako tayari kwa mtindo wa uchezaji wa raia huyo wa Cameroon.

“Bila shaka yeye ni kipa wa kisasa sana na mambo yako hivyo siku hizi,” Foster alinukuliwa nchini Uingereza.

“Ikiwa Manchester United walitaka kuimarika na kupiga hatua, basi walihitajika kusaini Onana. Hakuna mjadala kuhusu hilo. Hata hivyo, sijui iwapo wachezaji wenzake wako tayari kwa uchezaji wake wa kila mara kuanzisha mpira kutoka nyuma, akifanya majukumu ya kipa na difenda. Nimeona anavyotoka sana langoni na mpira na sina uhakika ikiwa wachezaji wenzake wako tayari kwa aina hiyo ya mchezo. Nasubiri kuona mambo yatakavyokuwa msimu ujao, ingawa sidhani kama ni kitu cha busara,” alisema Foster.

Kipa huyo anayechezea Wrexham katika ligi ya daraja la tatu nchini Uingereza pia alionya Onana kuhusu presha kali inayomsubiri pamoja na matarajio makubwa kutoka kwa klabu na mashabiki kwa sababu yeye sasa ni kipa nambari moja.

Alisifu jinsi De Gea alivyodhibiti hali hiyo katika kipindi cha miaka 12 akiwa uwanjani Old Trafford.

“Ningekuwa kocha wa United, ningemkwamilia David kwa angalau msimu mmoja zaidi,” alisema Foster.

  • Tags

You can share this post!

Wajumbe 3 wa mapatano

Drama mzoga wa paka ukiondolewa dukani

T L