Habari za Kitaifa

Pendekezo simu zizimwe wakati wa KCSE kuzuia udanganyifu

Na WINNIE ATIENO September 23rd, 2024 2 min read

WALIMU wakuu wa shule za upili wamependekeza mikakati ya kudhibiti udanganyifu kwenye mitihani ya kitaifa ikiwemo kuzuia matumizi ya simu na kubadilisha wasimamizi.

Haya yanajiri huku ikiwa imesalia mwezi mmoja kabla ya mitihani ya kitaifa kuanza ikiwemo mitihani ya kitaifa kwa shule za sekondari (KCSE).

Muungano wa Walimu Wakuu wa Sekondari Nchini (Kessha) umependekeza mikakati kabambe ya kuimarisha usalama na ulinzi wakati wa majaribio hayo yanayotumika kuwapandisha vyeo.

Walimu wakuu sasa wanaitaka serikali kufunga mawimbi ya simu wakati wa KCSE, wakisema hatua hii itazuia mawasiliano wakati wa mitihani.

“Kubadilisha waangalizi pia kutapunguza hali ya kuzoeana na uwezekano wa kushirikiana. Kamera za CCTV ziwekwe kumulika ukumbi wa mitihani ili kuzuia udanganyifu,” ilisema nakala ya udadisi uliofanywa na walimu wakuu.

Kwa miaka mingi, watahiniwa wamekuwa wakinaswa kila mara na simu wanazotumia kudanganya.

Udadisi uliofanywa kuhusu madai ya udanganyifu katika KCSE 2022, kwa mfano, ulifichua kuwa wanafunzi walitumia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Telegram na Facebook kuibia mitihani.

Walimu wakuu vilevile wametoa wito wa kubuniwa upya kwa Tume inayosimamia Mitihani Nchini (KNEC) ili kuwezesha kutekeleza shughuli zake kwa njia huru wakisema hatua hiyo itachangia pakubwa kuhakikisha uadilifu wa mitihani ya kitaifa.

“Uhuru huhakikisha michakato ya mitihani ya kitaifa isiyo na ubaguzi na hupunguza kuingiliwa na washirika kutoka nje,” walisema maafisa wa Kessha wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kitaifa Willy Kuria.

Aidha, walimu wakuu wamependekeza uzingatiaji wa sheria inayopiga marufuku uorodheshaji wa watahiniwa na shule wakisema hatua hiyo itaondoa shinikizo la kuvuruga matokeo.

Wameunga mkono vilevile pendekezo la Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) la kushirikisha walimu wa sekondari kama waangalizi badala ya mfumo unaotumika kwa sasa ambapo mitihani hiyo husimamiwa na walimu wa shule za msingi.

“Walimu wa sekondari wana uelewa bora kuhusu wanafunzi wa shule za upili wanaowasimamia. Walimu wa sekondari wanaweza kuwa na ujasiri zaidi na kuwadhibiti vyema watahiniwa kutokana na hali ya kutagusana nao kila wakati,” alisema Bw Kuria.