Habari za Kitaifa

Pigo kwa Masengeli Korti ikikataa kusikiliza ombi lake

Na SAM KIPLAGAT September 18th, 2024 1 min read

MAHAKAMA ya Rufaa imekataa kusikiliza ombi la Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na kulisukuma hadi wiki ijayo.

Bw Masengeli alitaka kesi hiyo isikilizwe haraka katika juhudi zake za kukwepa hukumu ya Mahakama Kuu iliyomfunga jela miezi sita.

Hukumu ya kumtupa jela mkuu huyo wa polisi, ilitolewa Ijumaa, Septemba 13, 2024 na Jaji Lawrence Mugambi wa Mahakama Kuu baada ya afisa huyo kukosa kufika mahakamani mara nane alivyoagizwa.

Majaji Gatembu Kairu, Weldon Korir na Aggrey Muchelule waliagiza kesi hiyo kushughulikiwa wiki ijayo kufuatia ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) la kutaka muda zaidi wa kuijibu.

Kupitia kwa wakili wake Cecil Miller, Bw Masengeli alidai kwamba alienda kortini akikusudia mchakato wa dharura, kwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi alimpa muda wa hadi Septemba 20, ambapo kifungo cha miezi sita kitaanza kutumika.

‘Tumezingatia ombi la LSK na tunaona kuwa ni ombi linalofaa kwani wanahitaji muda wa kutosha kuwasilisha majibu yao,’ Jaji Kairu alisema katika uamuzi huo.

Majaji hao waliagiza kwamba maombi yote mawili, moja lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dorcas Oduor akipinga hukumu ya Masengeli na lile la Masengeli, kusikilizwa kwa pamoja.

Kwenye ombi hilo, Bw Masengeli alisema kumtaka afike mbele ya Jaji Mugambi ili kuepuka kifungo cha nje, hakuruhusiwi kwani kunaweza kuathiri uadilifu na kesi hiyo ya rufaa kusikilizwa kwa dharura.

Katika rufaa hiyo, Bw Masengeli alisema jaji wa Mahakama Kuu alimhukumu bila kusikizwa.

Aidha, alisema mahakama ‘ilipuuza’ hati ya kiapo inayoeleza msimamo wa polisi kuhusu ndugu waliopotea, Jamil na Aslam Longton na mwanaharakati Bob Micheni Njagi na kusisitiza kuhudhuria kwake binafsi.

‘Kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ulinishutumu bila kusikilizwa, na kukiuka kwa kiasi kikubwa haki yangu isiyoweza kupuuzwa ya kusikilizwa kama inavyotolewa chini ya Kifungu cha 25 cha katiba,’ aliongeza.

Aidha alisema uamuzi wa Jaji Lawrence Mugambi huenda uliathiriwa na mambo mengine.