Habari za Kitaifa

Polisi wapata nyongeza ya donge nono

Na KAMORE MAINA September 6th, 2024 1 min read

MAAFISA wa polisi wameongezewa mishahara utekelezaji wa sheria ya kuwapandisha vyeo ukisitishwa hadi kuteuliwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi.

Waajiriwa wapya katika huduma hiyo wamepata nyongeza ya mishahara ya Sh4,000 huku nyongeza ya juu zaidi ya Sh21, 000 ikiendea maafisa wakuu katika vyeo vya juu.

Alhamisi, Septemba 5, 2024, Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC)  pia ilitangaza kusimamisha kwa sheria ya kuwapandisha vyeo maafisa wa polisi.

Baadhi ya maafisa wa polisi walioajiriwa 1957 hadi sasa wamepandishwa vyeo kupitia vyeo vilivyotangazwa na kaimu IG Gilbert Masengeli ambavyo pia vinakuja na nyongeza za mishahara.

Bw Eliud Kinuthia, mwenyekiti wa tume hiyo, alikataa kufichua kiasi cha pesa ambacho Serikali itatumia kwa maafisa ambao wamepandishwa vyeo.

Akihutubia wanahabari katika afisi za tume hiyo jijini Nairobi, Bw Kinuthia alisema tume yake imesitisha upandishaji vyeo hadi Bw Douglas Kanja aliyeteuliwa na IG achukue wadhifa huo.

“Tume ilimhimiza kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi kusitisha kwa muda upandishaji vyeo maafisa wa polisi tunaposubiri uteuzi wa Inspekta Jenerali,” Bw Kinuthia alisema.

Alisisitiza kuwa upandishaji vyeo uliofanywa na Bw Masengeli ulifuata taratibu na kukanusha madai ya upendeleo.

“Tuko wazi kwa ukaguzi wowote na hatutasita kuangazia uamuzi wowote ambao hauafiki mwongozo,” Bw Kinuthia alisema.