Habari

Rais Kenyatta afanya mabadiliko katika baraza la mawaziri

March 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BALOZI Amina Mohamed ndiye Waziri mpya wa michezo wa Kenya baada ya Rashid Echesa kupigwa kalamu Machi 1, 2019.

Echesa ameangukiwa na shoka katika teuzi za serikali zilizofanywa na Ikulu ya Rais, Ijumaa. Amina, 57, alihudumu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni kutoka Aprili 23, 2013 hadi Januari 26, 2018, alipohamishiwa Wizara ya Elimu kabla ya kuteuliwa Ijumaa kuongoza Wizara ya Michezo.

Echesa aliteuliwa kuongoza Wizara ya Michezo mnamo Januari 26, 2018 akisubiri kuhojiwa kabla ya uteuzi huo kuidhinishwa Februari 12 mwaka 2018. Ripoti wakati huo zilienea kwamba Echesa atetemwa.

Hata hivyo, alifaulu kujaza nafasi ya Dkt Hassan Wario. Naibu Rais William Ruto alilazimika kutetea uteuzi wa Echesa alipokuwa na sherehe ya kurejea nyumbani katika eneo bunge la Mumias mnamo Machi 13, 2018.

Echesa alihudumu kama waziri kwa mwaka mmoja kabla ya kutemwa Machi 1, 2019.

Sababu kuu ya Echesa kutaka kutemwa Februari 2018 ilikuwa kutokana na kiwango chake cha chini cha masomo.

“Echesa aliacha kusoma katika darasa la saba,” vyombo vya habari viliripoti Februari 12.

 

Rashid Echesa wakati akiwa Waziri wa Michezo na Sanaa, ahutubu katika Shule ya Sekondari ya Navakholo, Kakamega Desemba 29, 2018. Picha/ Isaac Wale

Inasemekana Echesa alihudhuria Shule ya Msingi ya Shibale mjini Mumias kutoka mwaka 1990 hadi 1997 kabla ya kuacha kusoma kutokana na ukosefu wa karo.

Wakati huo, Kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale, aliitisha mkutano wa dharura wa Wabunge wote wa chama cha Jubilee pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kuunga mkono shughuli ya kumtema Echesa kutoka orodha hiyo.

“Echesa alishindwa kuelezea kinagaubaga kiwango chake cha elimu, lakini wasifu wake unaonesha aliacha shule akiwa katika darasa la saba,” ripoti hizo zilisema.

Echesa alijaza nafasi ya Wario, ambaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Austria.

Wanamichezo wengi pia hawakuridhika na Wario aliyehudumu kama Waziri wa Michezo, Utamaduni na Sanaa tangu mwaka 2013 kabla ya Echesa kuchukua usukani.

Katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho Echesa amehudumu kama waziri, amehusishwa na uovu kadhaa ukiwemo ulanguzi wa wanawake kutoka Pakistan mnamo Januari mwaka huu na uchapishaji wa picha feki za Seneta wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala akiwa uchi Oktoba mwaka 2018.